Na Tiganya Vincent-Mahakama-Katavi
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amesema ili kutekeleza Dira ya
Mahakama ya utoaji haki kwa wakati, Mahakama ya Tanzania ilijiwekea viwango vya
muda wa usikilizaji na umalizaji wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama ili kuhakikisha
wananchi wanapata haki zao kwa wakati.
Mhe.
Siyani ametoa kauli hiyo leo tarehe 18 Januari, 2023 katika Viwanja vya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa majengo
mapya ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Songwe na Lindi.
Alisema
kwa Mahakama Kuu, muda wa
kusikiliza mashauri haupaswi kuzidi
miezi 24, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya
ukomo wa muda wa kusikiliza mashauri yanayofunguliwa haupaswi kuzidi miezi 12 na Mahakama za Mwanzo ni miezi sita.
Jaji
Kiongoziu alisema kuwa pamoja kujipangia muda huo, kasi ya usikilizaji wa
mashauri imekuwa ikiongezeka mwaka hata mwaka ambapo msukumo
mkubwa umewekwa pia kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA)
katika
usikilizaji wa mashauri.
“Ni matumaini yangu kuwa
Mahakama nilizozindua leo zitazingatia ipasavyo miongozo yote inayohusu muda wa
usikilizaji wa mashauri na kuwezesha wateja kupata haki kwa wakati” aliagiza.
Aidha,
Mhe.
Siyani alisema kwa
kuzingatia mafanikio yaliyopatikana kwenye eneo hilo, viwango hivyo vya ukomo wa muda wa usikilizaji mashauri
kuwepo mahakamani vilivyowekwa
takribani miaka kumi iliyopita, sasa vimepitwa na wakati.
“Ninajua kwamba ziko
Mahakama mbalimbali nchini na hasa Mahakama za Mwanzo ambazo zimeshusha ukomo
huu wa muda hadi miezi mitatu. Aidha, Kanda nyingi za Mahakama Kuu nchini nazo
tayari zimeanza kujitangaza kutokuwa na mashauri ya muda mrefu. Bila shaka huu
ni wakati muafaka sasa kwa Mahakama kujitathmini upya ili kuona kama viwango
hivyo bado vinaendana na dira yake ya kutoa haki kwa wakati,” alisisitiza.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel amesema miradi mitatu hiyo imegharimu zaidi ya bilioni mbili hadi
kukamilika na imeshaanza kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo husika.
Naye
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe Geofrey Pinda amesema Mahakama ya
Tanzania imeboresha huduma mbalimbali na kupunguza malalamiko kwa wananchi, hivyo
serikali itaendelea kuboresha miundombinu yake ikiwemo ujenzi wa Mahakama za
mwanzo katika tarafa ambazo hazina Mahakama za Mwanzo ili kuboresha utoaji wa
huduma kwa wananchi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiwasili katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi kwa ajili ya uzinduzi wa Mahakama hizo tatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni