Na Waandishi wetu-Mahakama -Katavi
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustapher Siyani ametoa wito kwa watumishi kuhakikisha uboreshaji wa miundominu
ya majengo ya Mahakama inakuwa kielelezo cha huduma bora kwa wananchi.
Mhe Siyani ametoa wito huo leo tarehe 18 Januari,
2023 katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi wakati wa uzinduzi wa
majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi Lindi, Songwe na Katavi.
Alisema uzuri wa muonekano na ubora wa
miundombinu unatarajiwa kuwa uendane na
wajibu ambao Watanzania wamekasimu kwa Mahakama.
“Msiwaangushe Watanzania kwa kuendekeza
ubinafsi, rushwa na upendeleo. Haya ni magonjwa ambayo tiba yake ya kwanza na
kamili inapaswa kutoka miongoni mwenu wenyewe,” alisisitiza.
Alisema kuwa watumishi wa Mahakama wanapotumia
majengo hayo wakumbuke kwamba yanatokana na kodi za Watanzania ambao watakuja
kutafuta haki mbele yao.
Mhe. Siyani aliwataka watumishi watakaohudumu
katika majengo hayo kuyatunza ili yadumu na wanatakiwa kuchapa zaidi kazi ili
wajenge imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.
Jaji Kiongozi alisema uzinduzi wa Mahakama hizo tatu
za Hakimu Mkazi Katavi, Songwe na Lindi ni matokeo ya uwezeshwaji unaoendelea
kufanywa na Serikali pamoja na usimamizi na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
Miaka Mitano wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu unaofanywa na watumishi wa
Mahakama.
“Naomba nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali
kwa kuendelea kutenga fedha zinazowezesha maboresho makubwa yanayoendelea mahakamani
na kipekee, nimshukuru sana Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa
kuendelea kuweka misingi mizuri inayoiwezesha Mahakama kujenga miundombinu yake
na hivyo kuwa na mazingira mazuri yanayoiwezesha kutimiza wajibu wake,”alisema.
Alisema lengo la Mahakama ya Tanzania ni
kuhakikisha kuwa huduma inazopaswa kuzitoa zinawafikia wananchi katika kila
Mkoa.
Mhe. Siyani alisema hadi kufikia mwezi Septemba,
2022 tayari Mahakama imefikisha huduma za Mahakama ya Hakimu Mkazi katika mikoa
yote 26 ya Tanzania Bara na kuongeza kuwa kati ya Wilaya 139, Mahakama
imepeleka huduma zake katika Wilaya 134.
Alisema Wilaya tano zilizobaki ni Ubungo,
Chamwino, Mkalama, Ikungi na Sikonge hazifanyi kazi, bali zinapata huduma ya
Mahakama katika Wilaya za jirani kwa kuwa na mamlaka ya pamoja (concurrent
jurisdiction).
Jaji Kiongozi aliongeza kuwa kwa upande wa
Mahakama za Mwanzo, malengo ya Mahakama ya Tanzania ni kuzifikia kata zote
3,956. Alisema kuwa hata hivyo, mpaka sasa huduma za Mahakama zinapatikana
katika kata 960 pekee kote nchini.
Mhe. Siyani alisema katika mwaka fedha wa
2022/2023, Mahakama inakusudia kujenga Mahakama za Mwanzo mpya 60 katika maeneo
mbalimbali nchini.
Alisema kuwa majengo hayo yatasaidia kusogeza
huduma za utoaji haki karibu na wananchi na hivyo kuongeza kasi ya utekelezaji
wa nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Upatikanaji na Utoaji Haki
kwa wakati.
Aidha, Jaji Kiongozi huyo alisema ujenzi wa
Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa ya Katavi, Songwe na Lindi, kutasaidia
wakazi wa maeneo hayo kupunguza umbali kufuata huduma ya Mahakama lakini zaidi
kuharakisha kasi ya usikilizaji wa mashauri.
Alisema kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Katavi, wananchi wapatao 738,237 walilazimika kufuata huduma hiyo
katika Mkoa wa Rukwa takribani Kilomita 250 kutoka Mpanda.
Alisema umbali huo mkubwa wa kufuata huduma za
Mahakama uliwafanya wananchi wengi kutumia fedha nyingi na muda mrefu na
kuongeza kuwa wananchi waliokuwa wakitoka Mpanda kwenda mkoani Rukwa
walilazimika kulala Sumbawanga ili kesho yake wapate huduma kutokana na umbali
huo wa kilomita 250 uliofanya kuwa vigumu kwao kwenda na kurudi.
Mhe. Siyani alisema kwa wastani mwananchi mmoja
aliyekuwa na shauri lolote katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Rukwa kutokea
Mpanda, alilazimika kutumia zaidi ya Tshs. 100,000/= kwa safari moja.
Aliongeza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama
ya Hakimu Mkazi Songwe, wananchi walipaswa kusafiri umbali wa kilomita 75
kufuata huduma ya Mahakama na kulazimika kutumia kiasi cha Tsh. 80,000 kwa
safari moja.
Mhe. Siyani alisema kuwa umbali na gharama
viliwanyima baadhi ya wananchi wa maeneo hayo nafasi ya kufaidi huduma za haki.
Alisema hali hii ilirudisha nyuma juhudi za wananchi kujikwamua kiuchumi na
kuwakatisha wengi tamaa na hivyo kutofuatilia mashauri yao.
Alisema uzinduzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Lindi, Katavi na Songwe, utasaidia kumaliza changamoto za umbali, muda na
gharama, lakini kubwa zaidi kuharikisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wa Mikoa
hiyo.
Jaji Kiongozi alisema pia kuwa hayo yote
yanafanyika kama sehemu ya jitihada za Mahakama za kusogeza huduma zake karibu
na wananchi na hivyo kuimarisha imani yake kwa umma.
Jaji Kiongozi alisema pia kuwa hayo yote yanafanyika kama sehemu ya jitihada za Mahakama za kusogeza huduma zake karibu na wananchi na hivyo kuimarisha imani yake kwa umma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiwasili katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi kwa ajili ya uzinduzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Lindi, Songwe na Katavi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Sumbawanga, Mhe. Dustan Ndunguru akizungumza katika hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni