Na Eunice Lugiana-Mahakama, Pwani
Katika kuelekea uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini,
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha mkoani hapa imeandaa maandamano makubwa
yatakayowashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa Mahakama ili kuazimisha shughuli
hiyo muhimu.
Akiongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake
leo tarehe 20 Januari, 2023, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Joyce
Mkhoi amesema maandamano hayo yataanzia kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kibaha nakuishia kwenye viwanja vya Mailimoja stendi ya zamani.
“Katika kuelekea Wiki ya Sheria na kilele ya Siku
ya Sheria, elimu za kisheria zitatolewa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kibaha
na eneo la Magindu ambalo lipo mbali kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi,” alisema.
Akifafanua kauli mbiu ya mwaka huu “Umuhimu wa
utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu; Wajibu
wa Mahakama na wadau,” Mhe. Mkhoi amesema kauli mbiu hiyo imejikita zaidi
kupunguza msongamano wa mashauri mahakamani na pia kuweka amani baina ya
wadaawa.
Hakimu huyo amebainisha kuwa mashauri
yanamalizika kwa njia ya usuluhishi huleta amani tofauti na kusikiliza
kesi mpaka mwisho ambako kunaweza kunaleta
uadui. Kadhalika, alisema usuluhishi unaoka muda na fedha pia kwa wadaawa.
Mhe. Mkhoi ameeleza kuwa jamii imekua na
mwitikio mdogo kujua au kufanya usuluhishi licha ya kwamba kuna Mabaraza ya Kata
ya usuluhishi, Mabaraza ya Wilaya ya usuluhishi pamoja na Baraza la Usuluhishi
la masuala ya kazi.
Akijibu swali kuhusu mashauri yanayofunguliwa na
kumalizika kwa mwaka, Mhe. Mkhoi amesema kwa Mkoa wa Pwani mashauri ya jinai ni
mengi zaidi kuliko yale ya madai.
Amesema kwa mwaka uliopita mashauri
yaliyofunguliwa yalikua 153 na yaliyosikilizwa yalikuwa 244. Takwimu hizi
zinajumuisha na mashauri yaliyobaki mwaka juzi ambayo ni 139, hivyo mwaka huu
umeanza na mashauri ya zamani 48.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni