Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe ametoa wito maalum kwa
wananchi wa Kanda hiyo kuitumia ipasavyo wiki ya sheria ili kutibu kiu yao ya
kuelimishwa juu ya masuala mbalimbali yanayoilenga Mahakama na mifumo yake.
Jaji Ngwembe alitoa kauli
hiyo hivi karibuni katika mkutano na Vyombo vya Habari na kuzungumzia namna
Mahakama Kanda ya Morogoro ilivyojipanga kuadhimisha Wiki ya Sheria ambayo
inatarajiwa kuzinduliwa hapo tarehe 22 Januari, 2023 kitaifa jijini Dodoma.
Alisema kuwa wamejipanga
vizuri kuhakikisha elimu ya sheria inawafikia wananchi wengi zaidi. “Baada ya
uzinduzi tutaanza kutoa elimu ya sheria kwa wananchi, tena elimu hii itatolewa
bila mwananchi kuchangia gharama yeyote, garama pekee atakayoitumia Mwananchi
huyu ni kutoka nyumbani mpaka vilipowekwa vituo vya utoaji elimu,” alisisitiza
Mhe. Ngwembe.
Aidha, alieleza kuwa Kanda
ya Morogoro itajikita zaidi kutoa elimu juu ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya
usuluhishi katika Mahakama, ulinzi wa mtoto tangu akiwa tumboni mpaka
atakapofikisha umri wa kutambulika kama mtu mzima na utatuzi wa migogoro ya
ndoa na miradhi.
Mhe.Ngwembe alisema kuwa
wananchi wataelimishwa pia kuhusu makosa ya kijinai, ikiwemo kupatikana na nyara
za Serikali, makuzi na walezi ya vijana wawapo shuleni, mfumo wa Mahakama
kuanzia Mahakama ya Mwanzo mpaka Mahakama ya Rufaa ili mteja ajue shauri lake
linapaswa kupelekwa Mahakama ipi, kazi ya Mabalaza ya Ardhi pamoja na mada
nyinginezo.
Aliwaomba wananchi kufika
kwenye vituo vya kutolea elimu kwani sambamba na kujifunza mambo mengine pia
watapata kufahamu namna Mahakama ilivyojipanga na inavyotumia usuluhishi katika
kutatua migogoro mbalimbali inayofikishwa mahakamani kama inavyosema kauli mbiu
ya Wiki na Siku ya Sheria.
“Kupitia kauli mbiu hii
napenda kusema kuwa Mahakama yetu ya Tanzania imelitazama hili kwa jicho la
kipekee sana na sisi tutasisitiza zaidi usuluhushi na sio mashindano mahakamani
kwakuwa njia ya usuluhishi ikitumika, kila mmoja hutoka akiwa mshindi na hivyo kuendeleza
mahusiano bora yaliyokuwepo”, alisema.
Akielezea kuwa wameandaa
bonanza litakalokuwa na michezo mbalimbali na linatarajiwa kufanyika tarehe 21
Januari, 2023 ili kuhamasisha wananchi kujitokeza siku ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria
na Bonanza hilo linatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Jamuhuri kuanzia saa
kumi na mbili asubuhi.
Wiki ya Sheria imekuwa
ikiadhimishwa kila mwanzo wa mwaka kote nchini na kwa upande wa mwaka huu
inategemewa kuzinduliwa tarehe 22 Januari, 2023 itaifa jijini Dodoma na
kuhitimishwa tarehe 01 Februari, 2023 huku kauli mbiu ikiwa “Umuhimu wa Utatuzi
wa Migogoro kwa njia ya Usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu: Wajibu wa
Mahakama na wadau.”
Kwa Upande wa Kanda ya
Morogoro, uzinduzi utaanza kwa maandamano kuanzia lilipo jengo la Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki kuelekea katika Kiwanja cha Ndege ambapo kutakuwa ndio
kituo mama cha kutolea elimu, huku mgeni rasmi akitegemewa kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro. Mara baada ya uzinduzi elimu itaendelea kutolewa katika vituo vvya Stendi
ya Msamvu, Stendi ya Mafiga, Soko la Chief Kingalu pamoja na kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki Morogoro.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni