Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Kamati maalumu iliyoundwa na Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof Elisante Ole Gabriel kuratibu shughuli za Wiki na
Siku ya Sheria kwa mwaka 2023 imeshawasili tayari jijini hapa kutekeleza jukumu
hilo.
Akizungumza katika Viwanja vya Nyerere Square mahali
kutakapofanyikia maonyesho wa Wiki ya Sheria, Katibu wa Kamati hiyo, Mhe.
Charles Magesa amesema maandalizi ya shughuli hiyo yanaendelea vizuri na
wajumbe wote wapo tayari kutekeleza jukumu walilopoewa.
"Wajumbe wote wa Kamati wapo Dodoma na kazi
inaendelea. Maadalizi kama unavyoona yanaendelea vizuri na ninaamini hadi
kufikia kesho tarehe 21 Januari, 2023 kila kitu kitakuwa kipo tayari,"
alisema Mhe. Magesa.
Wiki ya sheria inatarajiwa kuanza siku ya
Jumapili tarehe 22 Januari, 2023 kwa mate matembezi maalumu yatakayoanzia
katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma majira ya saa 12.00 asubuhi. Mgeni
rasmi atakayeongoza matembezi hayo na kufungua Wiki ya Sheria ni Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Akiongea na waandishi wa habari mkoani
Dar-es-Salaam hivi karibuni, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis
Juma aliwaomba wananchi wote katika mkoa wa Dodoma na maeneo ya jirani
kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho hayo.
Alisema kuwa wananchi watakaofika kwenye viwanja
hivyo watapata nafasi ya kutoa malalamiko, maoni na mapendekezo ya uboreshaji
wa huduma za Mahakama, hivyo ni matumaini yake na ya Mahakama ya Tanzania kwa
ujumla kuwa taasisi zote zinazosimamia Sheria zinazotoa nafasi ya usuluhishi
zitumie Wiki ya Sheria kutangaza hizo fursa za usuluhishi.
“Sambamba na Elimu ya Sheria na maonesho
yatakayofanyika Kitaifa katika Mji Mkuu wa Tanzania, Dodoma, utoaji wa elimu ya
sheria kwa umma na maonesho utaendelea pia katika Kanda za Mahakama Kuu, Mikoa
na Wilaya nchi nzima kama ilivyofanyika kwa miaka mingine,” alisema.
Aidha, Jaji Mkuu alisema kuwa wakati wa Wiki ya
Sheria elimu itatolewa kuhusu taratibu za ufunguaji wa mashauri hasa kwa njia
ya mtandao, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri
mbalimbali kama yale ya Ndoa na Talaka, Ardhi, migogoro ya Kazi pamoja na
utekelezaji wa hukumu, Sheria za Watoto na taratibu za mashauri ya mirathi.
“Vilevile wanananchi watapata fursa ya kujifunza
huduma zitolewazo na Mahakama inayotembea “Mobile Court” na Mahakama za Vituo
Jumuishi. Wananchi watakaotembelea mabanda ya Mahakama watapata fursa ya
kujifunza kwa kiasi gani Mahakama ya Tanzania imejipanga kutoa haki katika
Karne ya 21 kwa kutumia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA),” alisema.
Alisema katika maonesho hayo, elimu hiyo
itatolewa na Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili, Mahakimu pamoja na wadau wa
Mahakama, wakiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu
wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume
ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi,
Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Kwa mwaka huu, katika maadhimisho haya ya Wiki
ya Sheria na Siku ya Sheria, kauli mbiu itakuwa Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro
kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na
Wadau.
Kilele cha Siku ya Sheria kitafanyika tarehe 1
Februari, 2023 katika viwanja vya China Chinangali jijini hapa na mgeni rasmi
atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni