·Wananchi waalikwa kushiriki Wiki ya Sheria kote nchini
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Maandalizi kuelekea maadhimisho ya Wiki ya
Sheria kwa mwaka 2023 ambayo yatahusisha maonesho na utoaji wa elimu ya
kisheria bure kutoka kwa wadau mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania yemekamilika.
Akizungumza katika Viwanja vya Nyerere Square kutakapofanyikia
maadhimisho hayo, Katibu wa Kamati maalumu iliyoundwa kuratibu shughuli hizo,
Mhe. Charles Magesa amesema wameshakamilisha maandalizi yote.
“Kazi imekamilika. Tupo tayari kwa maonesho na tupo
tayari kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi wetu. Wadau wote wanaoshiriki
kwenye maonesho kama unavyoona mabanda yao wameshafika kwa ajili ya shughuli hii,”
amesema.
Mhe. Magesa amewaalika wananchi wote kufika
katika Viwanja vya Nyerere Square na kutembelea mabanda ambayo yameandaliwa na
wadau wa Mahakama ili kujionea shughuli wanazofanya na kupata elimu kwenye
maeneo mbalimbali ya kisheria.
Elimu itakayotolewa inahusu taratibu za
ufunguaji wa mashauri hasa kwa njia ya mtandao, sheria na taratibu zinazotumika
katika kuendesha mashauri mbalimbali kama yale ya Ndoa na Talaka, Ardhi,
migogoro ya Kazi pamoja na utekelezaji wa hukumu, Sheria za Watoto na taratibu
za mashauri ya mirathi.
Vilevile wanananchi watapata fursa ya kujifunza huduma
zitolewazo na Mahakama inayotembea “Mobile Court” na Mahakama za Vituo
Jumuishi, watajifunza jinsi Mahakama ya Tanzania imejipanga kutoa haki katika
Karne ya 21 kwa kutumia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA).
Katika maonesho hayo, elimu hiyo itatolewa na
Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili, Mahakimu pamoja na wadau wa Mahakama,
wakiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya
Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi,
Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Hivi karibuni, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Prof Elisante Ole Gabriel aliteua Kamati maalum kuratibu shughuli mbalimbali,
ikiwemo kufanikisha matembezi ya ufunguzi wa Wiki ya Sheria tarehe 22 Januari,
2023.
Kadhalika, Prof. Ole Gabriel aliitaka Kamati
hiyo kuratibu utoaji wa elimu ya kisheria kwa wananchi kwenye Viwanja vya
Nyerere Square kuanzia Januari 22 hadi 29, 2023 na kufanikisha Siku ya Sheria
itakayofanyika kitaifa tarehe 1 Februari, 2023 ambapo mgeni
rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan.
Wiki ya Sheria itakayofanyika kitaifa siku ya Jumapili
tarehe 22 Januari, 2023 itaanza kwa matembezi maalumu yatakayoanzia katika
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma majira ya saa 12.00 asubuhi na kuongozwa
na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Sambamba na Elimu ya Sheria na maonesho
yatakayofanyika Kitaifa katika Mji Mkuu wa Tanzania, Dodoma, utoaji wa elimu ya
sheria kwa umma na maonesho utaendelea pia katika Kanda za Mahakama Kuu, Mikoa
na Wilaya nchi nzima kama ilivyofanyika kwa miaka mingine.
Kwa mwaka huu, katika maadhimisho haya ya Wiki
ya Sheria na Siku ya Sheria, kauli mbiu itakuwa Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro
kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na
Wadau.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni