Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Morogoro leo tarehe 21 January, 2023 imefanya bonanza la michezo
mbalimbali lililovuta hisia za wakazi wa mji ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha
wananchi kujitokeza kushiriki siku ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria inayotarajiwa
kuzinduliwa hapo kesho tarehe 22 January, 2023.
Bonanza hilo lilifanyika
katika Uwanja wa Michezo wa Jamuhuri ulipo mkoani hapa huku mgeni rasmi akiwa
ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul
Ngwembe aliyeongoza mamia ya wananchi wa Mkoa huo kushiriki katika michezo hiyo
iliyoandaliwa.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi, Mhe. Ngwembe alisema kuwa ni wakati sasa wananchi kuwa karibu na
Mahakama ndio maana michezo hiyo haikumbagua mtu yeyote ambapo wote aliruhusiwa
kujiandikisha kushiriki. Aliongeza pia kuwa safari hii Mahakama itajikita zaidi
katika kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi na sio kutumia hukumu katika
kila jambo.
Aidha, Mhe. Ngwembe
alitoa angalizo kwa wananchi kwamba Mahakama haitaacha kazi yake ya msingi ya
kutoa hukumu bali itatoa hukumu kwa mashauri yatakayobidi kutolewa hukumu kwa mashauri
yaliyoshindwa kufikia muafaka kwa njia ya usuluhishi.
Naye mshiriki toka klabu
ya Moro Runners, Albert Nziolela alitoa shukrani zake kwa uongozi wa Mahakama
kwa kuandaa michezo hiyo kwani imesaidia kuwaleta karibu na Mahakama na kuongeza
kuwa wamegundua Mahakama sio adui bali ni Rafiki. Amesema wataitumia nafasi ya Wiki
ya Sheria kufika katika mabanda ya Mahakama ili wajifunze zaidi.
Bonanza la michezo
lilianza kwa mbio fupi za kilomita tano ambazo ilikuwa na washiriki toka klabu
zote za kukimbia zilizoko Morogoro mjini, washiriki toka taasisi na mabenki,
wananchi, wadau na watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro ambapo walishiriki
michezo mbalimbali, ikiwemo kuvuta kamba, mbio za mita mia nne, kukimbiza kuku,
kukimbia ndani ya magunia, mpira wa kikapu na mpira wa miguu.
Aidha katika michezo hiyo,
washindi walipata bahati ya kutunukiwa vyetu vya kutambua mchango wao na baada
ya michezo wote walioshiriki walipata nafasi ya kupata chakula cha pamoja na mgeni
rasmi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mbando akifuatilia matukio mbalimbali uwanjani hapo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni