Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 22 Januari, 2023 ameongoza maelefu
ya Watanzania kwenye matembezi maalum yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania
kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria inayoambatana na utoaji wa elimu ya
kisheria kwa wananchi.
Matembezi hayo yaliyoshirikisha viongozi mbalimbali
wa Mahakama ya Tanzania, akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Majaji
wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu na watendaji wengine yalianzia katika
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kumalizikia katika Viwanja vya Nyerere
Square.
Mongoni mwa viongozi wengine ambao wameshiriki kwenye
matembezi hayo ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary
Senyamule, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabiri Shekimweri na wajumbe wa Tume
ya Utumishi wa Mahakama.
Wadau mbalimbali wa Mahakama, wakiwemo Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa
ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama
cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza na Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS) wameshiriki katika maandamano hayo kwa wingi.
Vikundi mbalimbali vya kukimbia (jogging) pamoja
na bendi ya JKT Makutupora vimeshiriki katika kunogesha matembezi hayo.
Wananchi walianza kujitokeza kwenye matembezi hayo majira ya saa 11 asubuhi ambayo
yalianza majira ya saa 12 hivi baada ya viongozi mbalimbali kufika katika eneo ambalo
yalianzia.
Ilichukua takribani saa moja na nusu hivi kwa viongozi
na wanachi kuwasili katika Viwanja vya Nyerere Square ambapo Makamu wa Rais
alianza kutembelea Banda la Kituo cha
Usuluhishi na kupatiwa maelezo namna kinavyofanya kazi na Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Wanjah Hamza.
Katika maelezo yake mafupi, Mhe. Wanjah
amemweleza Makamu wa Rais kuwa Kituo hicho kimefanikiwa kusuluhisha mashauri
mbalimbali yanayopokelewa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam
na kuokoa zaidi ya billioni 12 za Kitanzania, fedha ambazo zingelipwa na wadaawa
kama wengeamua kumaliza migogoro yao kwa njia ya kawaida ya kusikiliza
mashauri.
Mhe. Dkt. Mpango ameonyesha kufurahishwa na
utendaji wa Kituo hicho, hivyo kuhimiza Mahakama ya Tanzania kuendelea kutoa
elimu kwa wananchi kuhusu utaratibu wa kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi,
hatua ambayo ina manufaa makubwa, ikiwemo kumaliza mashauri kwa muda mfupi na
kwa gharama nafuu.
Makamu wa Rais pia alitembelea mabanda mengine
ikiwemo lile Usimamizi Mashauri, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
pamoja na Wizara ya Ardhi. Akiwa katika banda la Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Mpango
alieleza jinsi migogoro ya ardhi inavyosumbua wananchi na kuagiza Mabaraza ya
Ardhi kujitazama upya kwa vile utendaji kazi wake hauridhishi.
Baada ya kutembelea mabanda ya maoenyesho yaliyoandaliwa
na wadau mbalimbali, Makamu wa Rais aliongozana na viongozi wengine kuelekea
kwenye jukwa kuu ambapo wimbo wa Taifa ulipigwa kabla ya shughuli zingine kwenye
ufunguzi huo wa Wiki ya Sheria kuendelea.
Sambamba na Elimu ya Sheria na maonesho
yatakayofanyika Kitaifa katika Mji Mkuu wa Tanzania, Dodoma, utoaji wa elimu ya
sheria kwa umma na maonesho utaendelea pia katika Kanda za Mahakama Kuu, Mikoa
na Wilaya nchi nzima kama ilivyofanyika kwa miaka mingine.
Kwa mwaka huu, katika maadhimisho haya ya Wiki
ya Sheria na Siku ya Sheria, kauli mbiu itakuwa Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro
kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na
Wadau.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni