Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa rai kwa Mahakama na Wadau wake kuelimisha
wananchi kuhusu njia bora zaidi ya utatuzi wa migogoro yao na hususani njia ya usuluhishi
ambayo ina faida nyingi ikiwemo kuokoa muda.
Akizungumza mapema leo tarehe 22 Januari, 2023, katika
hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini
Dodoma, Mhe. Dkt. Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo amesema
kuwa, kuna umuhimu wa kuwa na mfumo thabiti wa kutatua migogoro ili kuokoa muda
unaotumika katika uendeshaji wa kesi kwa njia ya kawaida.
Kauli mbiu ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu ni;
Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu:
Wajibu wa Mahakama na Wadau.
“Napenda nikiri wazi kwamba, nimefurahishwa na Kaulimbiu
ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu ambayo inahimiza Usuluhishi kama njia mojawapo
ya utatuzi wa migogoro ambayo kimsingi una faida nyingi ikiwemo kuokoa muda,
kupunguza mlundikano wa mashauri, kukuza uchumi wa Taifa na nyingine,” amesema
Makamu wa Rais.
Aidha, Mhe. Dkt. Mpango amewaomba pia Viongozi wa dini
kuwakumbusha waumini wao kuhusu umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya
usuluhishi huku akiwahamasisha wananchi kutembelea mabanda ya Mahakama na wadau
katika Maonesho ya wiki ya utoaji elimu ya sheria yanayoendelea nchi nzima.
Kadhalika, Mhe. Dkt. Mpango amempongeza Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kuuongoza vyema Mhimili wa Mahakama hususani katika kusimamia
uboreshaji wa huduma ikiwemo matumizi ya TEHAMA mahakamani, uboreshaji wa usimamizi
wa mashauri, miundominu ya majengo ya Mahakama na kadhalika.
“Naipongeza Mahakama ya Tanzania hususani Jaji Mkuu,
Mhe. Prof. Juma kwa kuendelea kuiongoza vyema Mahakama katika kuboresha huduma
zake, kwa kifupi naweza kusema ‘you have transformed Judiciary to the next level’”
amesisitiza Makamu wa Rais.
Kadhalika, Makamu wa Rais amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba kuihusisha Mahakama ya Tanzania kikamilifu katika Dira ijayo ya Taifa ambayo ipo kwenye mchakato wa kuandaliwa .
Hata hivyo, Mhe. Dkt. Mpango amewakumbusha Viongozi wa
Mahakama kuendelea kufanyia kazi changamoto kadhaa za Mahakama ambazo ni pamoja
na kuwawajibisha baadhi ya watumishi wa Mhimili huo ambao wanajihusisha na
vitendo cha rushwa na ukiukwaji mwingine wa maadili na nyingine.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma amesema kuwa, wananchi walio wengi bado hawafahamu
taratibu hizo na pia kuelewa ni namna gani sheria na taratibu zake zina
uhusiano na uchumi au zinavyoweza kuathiri shughuli zao za kila siku za
kijamii, kiuchumi, na uzalishaji mali.
“Mahakama inafahamu kwamba sio
wananchi wote tunaowahudumia wanafahamu vema haki na wajibu wao katika taratibu
za kupata haki zao pale ambapo migogoro itaibuka. Kwa sababu hiyo, Mahakama ya
Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa utoaji haki kila mwaka hutumia
maadhimisho ya wiki ya sheria kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi kufahamu
taratibu mbalimbali za kupata haki na pia kuwaelimisha juu ya haki na wajibu
wao katika kupata haki,”
amesema Mhe. Prof. Juma.
Akizungumzia suala la Usuluhishi, Mhe. Prof. Juma
amesema wananchi wana wajibu wa kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi huku
akitoa wito kwa wananchi kutembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria na hususani Mahakama
Kuu Kituo cha Usuluhishi ili kupata elimu na uelewa zaidi kuhusu njia hiyo
iliyosheheni faida lukuki kwa kufanya hivyo kutawapa nafasi ya
kufanya shughuli za uzalishaji na kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa Taifa.
“Ni muhimu wananchi wafahamu pia namna
ambavyo migogoro ya biashara, kazi au mikataba inayoweza kutokea kwa njia za
mitandao; na inavyoweza kutatuliwa (ikiwemo kwa njia ya usuluhishi) kwa njia ya
TEHAMA. Silaha
bora ya kupigania Haki ni kuelewa upatikanaji wa hiyo Haki unayopigania ipo
chini ya Sheria, Kanuni au Taratibu zipi,” amesisitiza Jaji Mkuu.
Ameongeza kwamba, utoaji elimu unatarajiwa
kutolewa kwa namna mbalimbali ikiwemo vipindi vya redio, midahalo, na maonesho
katika maeneo mbalimbali nchi nzima kwa kipindi chote cha maadhimisho lengo ni kuwafikia wananchi wengi hata
wale wa vijijini kadri inavyowezekana. Huku akitoa wito kwa wananchi kutumia fursa hii
muhimu kwao kufuatilia elimu itakayotolewa.
Maonesho haya yaliyozinduliwa leo yatafanyika kwa muda wa siku nane ambapo yanatarajiwa kukamilika tarehe 29 Januari, 2023 ambapo yatahitimishwa kwa kilele cha Siku ya Sheria itakayofanyika tarehe 01 Februari, 2023 huku mgeni rasmi wa siku hiyo muhimu anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kulia) akitoa ufafanuzi wa jambo mbele ya Mgeni rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (mwenye traki suti nyeusi) (na kushoto kwake mwenye tisheti nyeupe) ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakisikiliza kwa makini ufafanuzi wa jambo hilo wakati alipokuwa akikagua mabanda yatakayotumika kutoa elimu kwa umma kwa kipindi chote cha wiki ya sheria nchini na kuwasikiliza wadau
Mgeni rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (mwenye traki suti nyeusi) akitoa maelekezo kwa Viongozi wa Muhimili wa Mahakama akiwepo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel wakati alipokuwa akikagua mabanda yatakayotumika kutoa elimu kwa umma kwa kipindi chote cha wiki ya sheria nchini na kuwasikiliza wadau wa Mahakama.
Sehemu ya Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania na Serikali wakiwa wameketi jukwaa kuu wakati wa hafla ya uzinduzi wa wiki ya sheria nchini.
Sehemu ya Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania na Serikali wakiwa wameketi jukwaa kuu wakati wa hafla ya uzinduzi wa wiki ya sheria nchini.
Kwaya ya Mahakama ya Tanzania wakitumbuiza katika hafla ya uzinduzi wa wiki ya sheria nchini.
Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya Mahakama Kuu ya Wanakwaya wa Kwaya ya Mahakama ya Tanzania ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za hafla ya ufunguzi wa wiki ya sheria nchini.
(Picha na Innocent Kansha na Mary Gwera - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni