Na Waandhishi Wetu-Mahakama ya Tanzania
Wananchi nchini kote leo
tarehe 22 Januari, 2023 wamejitokeza kwa wingi kushiriki kwenye matembezi
maalum kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria huku Majaji Wafawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania katika maeneo mbalimbali wakitoa ujumbe mahsusi kwa Watanzania
kujitokeza na kupata elimu ya sheria itakayotolewa katika maonyesho yaliyoandaliwa
na wadau wa Mahakama.
Kutoka Mahakama Kuu Musoma, Fransisca Swai anaripoti
kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu
Mtulya, amewaasa wananchi kutumia wiki hii kujipatia elimu mbalimbali ya
kisheria na hasa juu ya haki za watoto, kwani watoto wengi wanatendewa mambo
yasiyofaa.
“Kama jamii tunayohaki ya kuwasaidia wananchi
na zaidi kutumia usuluhishi nje ya Mahakama katika kutatua migogoro katika
jamii zetu,” alisema na kisha aliwaalika wananchi kufika maeneo yote
yaliyoandaliwa katika Mkoa kwa ajili ya kupata elimu mbalimbali itakayotolewa
na Mahakama na Wadau.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Selemani Mzee ameipongeza Mahakama
kwa kauli mbiu ya mwaka huu na kuwaasa wananchi kutumia usuluhishi kama njia
kuu ya kutatua matatizo yao na kusisitiza njia ya usuluhishi inaleta amani,
maelewano na umoja katika jamii , hivyo kusaidia kuimarisha uchumi wa mtu mmoja
mmoja na taifa kwa ujumla.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Musoma, Mhe. Halfani Haule amewaasa wananchi kutumia usuluhishi kwa kuwa
utapunguza migogoro na kuleta amani. Kadhalika, ameishukuru Mahakama kwa namna
inavyoshirikiana na wadau katika kuhakikisha mashauri yanaamuliwa kwa wakati na
haki inatendeka, jambo ambalo linaloleta amani hasa katika Wilaya ya Musoma.
Kutoka Mahakama Kuu
Mbeya, Ibrahim Mgallah anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim ameongoza matembezi maalum
kuashiria uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria nchini kwa mwaka
2023. Katika uzinduzi huo yamefanyika matembezi kuanzia Mahakama Kuu Mbeya na
kuishia katika kituo cha mabasi Kabwe mahali itakapotolewa elimu ya sheria kwa
wananchi hadi tarehe 29 Januari, 2023.
Akizungumza katika baada
ya matembezi hayo, Mhe. Ebrahim aliwaeleza wananchi kuwa elimu ya sheria
itatolewa kupitia vyombo vya habari, maonesho, kutembelea shule mbalimbali na
magereza.
Aidha, aliwashauri
wananchi kutumia njia ya usuluhishi kutatua migogoro yao ili kuepuka kutumia
muda mwingi mahakamani badala yake watumie muda huo katika shughuli za
uzalishaji.
“Utatuzi wa migogoro ya
wananchi unapaswa kuzingatia njia za usuluhishi ili kupunguza ufuatiliaji wa
migogoro yao Mahakamani na badala yake muda huo wautumie kufanya shughuli za uzalishaji
na kukuza kipato ili kukuza uchumi wa taifa letu na wananchi wenyewe kwa
ujumla,” alisema Jaji Mfawidhi.
Naye Mkuu wa Wilaya
Mbeya, Mhe. Dkt. Rashid Chuachua ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuandaa
maudhui ambayo yanalenga kuimarisha zaidi umoja, amani, udugu na mshikamano kwa
Watanzania.
Naye Stephen
Kapiga-Mahakama Mwanza anaripoti kuwa maadhimisho ya Wiki ya Sheria yamefanyika
kwa mara ya kwanza katika Wilaya ya Ilemela, hivyo kuwaacha na butwa wananchi
wengi wa Kata ya Buswelu ambao hawakuwahi kuwaona Majaji wakitembea kwa miguu.
Maadhimisho haya
yalitanguliwa na maandamamo ya watumishi wa mahakama, wadau pamoja na wananchi
ambayo yaliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanania, Kanda ya
Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga. Maandamano hayo yalipokelewa na Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salumu Kalli.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Jaji Mfawidhi aliwashukuru wote kwa kuitikia na kukubali kujumuika na
Mahakama katika uzinduzi huo kwani ni fursa kwa wananchi kuweza kujifunza mengi
na kupata msaada wa kisheria.
“Napenda kuwakaribisha
wote muweze kufika na kupata huduma zetu na za wadau wetu. Umuhimu wa utatuzi
wa migogoro kwa njia ya usuluhushi ndilo jambo tunalohitaji kwa sasa kwani hii
inafanya wadaawa wote waondoke mahakamani wakiwa na amani na furaha,” alisema.
Nae Mhe. Kalli
aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuona umuhimu wa kutanguliza usuluhishi
kwani hii itasaidia kuokoa muda ambao wananchi walikuwa wakiuutmia kuja
mahakamani.
Kutoka Manyara, Christopher Msagati anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza ameongoza maandamano ya watumishi
wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Mahakama ya
Wilaya ya Babati, Mahakama za Mwanzo Babati na wananchi kwa ujumla kushiriki
katika maandamano maalum yaliyoandaliwa kuashiria uzinduzi wa Wiki ya Sheria
nchini.
Katika maandamano hayo
ambayo Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Lazaro Twange ameshiriki, wadau wa haki jinai
pamoja na wananchi wa Wilaya ya Babati wameshuhudia kufana kwa uzinduzi wa maadhimisho
ya Wiki ya Sheria nchini kwa Mwaka huu 2023 yaliyofanyika kwa mara ya kwanza tangu
kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Kanda mpya ya Manyara mnamo Mwezi Novemba mwaka
2022.
Katika uhafla hiyo, Mhe.
Kahyoza alimueleza Mkuu wa Wilaya lengo la kukutana ambalo ni kuelezea umuhimu wa
Wiki ya Sheria pamoja na kuwafanya wananchi watambue kuwa Mahakama ipo kwa
ajili yao, hususan kuwasaidia kupata haki zao za msingi.
Watu wote waliohudhuria
walipata nafasi ya kushuhudia maonesho mbalimbali yaliyoandaliwa na watumishi
wa Mahakama, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, TAKUKURU pamoja na TAWJA.
Aidha, umati ulikoshwa na namna ambavyo Mahakama ya Tanzania inavyojiboresha
katika miundombinu ya majengo na matumizi ya TEHAMA.
Kwa upande wake, Mhe.
Twange ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara. Mhe. Charles Makongoro alisema
kuwa katika taasisi ambazo zinakuwa katika matumizi makubwa ya TEHAMA ni pamoja
na Mahakama ambayo imekuwa mfano mzuri wa kuigwa na Taasisi zingine.
Naye Advela Kalunde kutoka Mahakama
Njombe ameripoti kuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liad Chamshama amewakaribisha wananchi wote kufika
katika viwanja vya Bakita kuanzia kesho kwa ajili ya kupata elimu mbalimbali
itakayotolewa na wadau mbalimbali katika viwanja hivyo mpaka tarehe 29 Januari,
2023.
Katibu tawala ambaye
alikua kiongozi wa maandamano hayo amewasii wananchi kufika katika viwanja
hivyo ili waweze kupata elimu ya sheria, huku akisisitiza kuwa kauli mbiu ya
mwaka huu inalenga kuondoa migogoro katika jamii.
Matembezi hayo yalianzia
katika viwanja vya Bank ya NBC Tawi la Njombe yakijumuisha wadau mbalimbali wa
Mkoa wa Njombe, wakiwemo Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa serikali, TAKUKURU, CMA,
Huduma kwa jamii, Mawakili, Watumishi wa Mahakama, Polisi, Magereza, vikundi
mabilimbali vya michezo pamoja na wanachi. Maandamano hayo yaliishia katika
viwanja vya shule ya Msingi Bakita.
Kwa upande wake Eunice kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha anaripoti kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Sarah
Msafiri amewataka wananchi kutenga muda wa kutembelea mabanda yanayotoa elimu
ya sheria. Amesema kuwa katika Wilaya ya Kibaha migogoro mingi ni ya ardhi
ambapo kumekua na uadui mwingi, hivyo amewaomba wananchi wapate elimu ili
waweze kutatua migogoro hiyo nje ya Mahakama.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya
amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hasasn kwa kutenga kiasi cha bilioni 96 za Kitanzania kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama
mbalimbali nchini, ikiwemo Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mkoa wa Pwani ambacho
kitajengwa katika Wilaya ya Kibaha. Amesema Kituo hicho kitachukua vitengo
vyote vinavyojihusisha na utoaji haki pamoja na Mahakama zote kuanzia Mahakama
ya Mwanzo mpaka Mahakama Kuu.
Awali, akimkaribisha mgeni
rasmi kuzungumza na wananchi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kibaha, Mhe. Joyce Mkhoi amesema usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama unaleta
uchumi mzuri na hivyo kupunguza umaskini kwa kutumia muda mrefu kuhudhuria
mahakamani kusikiliza kesi badala ya kufanya kazi nyingine za uchumi ili
kuongeza kipato.
Mhe. Mkhoi amesema Mahakama
pamoja na wadau wataweza kukumbusha wajibu wao katika kuhakikisha kesi ambayo inaweza kuisha kupitia usuluhishi basi ikaisha katika njia
hiyo badala ya kupoteza muda mwingi mahakamani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni