Na Faustine Kapama-Mahakama, Arusha
Mahakama
ya Tanzania imepokea maombi ya Wazabuni 138 katika utekelezaji wa miradi mipya,
ikiwemo ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki zaidi ya tisa na Mahakama za
Mwanzo 60 zitakazojengwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Hayo
yamebainishwa leo tarehe 3 Januari, 2023 na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Dkt Angelo Rumisha katika siku ya kwanza ya mafunzo maalumu
ambayo yameandaliwa kwa sehemu ya watumishi watakaochambua maombi hayo.
Mhe. Rumisha
amebainisha wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanafanyika katika Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo jijini hapa kuwa kwenye mradi wa maboresho awamu
ya pili Mahakama imepanga kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki agalau tisa na
Mahakama za Mwanzo ambazo ni 60 katika maeneo mbalimbali.
“Tumeanza
ratiba za manunuzi kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. Ujenzi wa Mahakama unataratibu
nyingi kwa mujibu wa taratibu za wenzetu wa Benki ya Dunia. Tunatafuta
wataalamu waelekezi ambao husaidia kuchora michoro na kusimamia ujenzi,” Mhe.Rumisha
alisema.
Ameeleza
kuwa tayari mtaalamu wa kuchora michoro ameshapatikana kwenye Vituo Jumuishi na
kwa sasa wanatafuta wataalamu elekezi kwa ajili ya kusimamia ujenzi huo. Mhe.
Rumisha amesema pia kuwa wanatafuta wataalamu elekezi kwa ajili ya kutoa
michoro na kusimamia ujenzi kwenye Mahakama za Mwanzo.
“Tarehe 29
Disemba, 2022 tulifungua zabuni na kwa mara ya kwanza yamepatikana maombi mengi
ambayo hayajawahi kuonekana kwenye utaratibu wa kimahakama. Kuna maombi 138 kwa
ajili ya kushauri kwenye michoro na usimamizi wa ujenzi huo,” amesema.
Amebainisha
ugumu wa kazi katika kuchambua maombi hayo kwa kuzingatia kuwa ni Wazabuni 10 pekee
ndio wanaotakiwa. Mhe. Rumisha amesema kuwa baada ya kupata maombi hayo na kwa
kuzingatia historia ya huko nyuma wakaona ni vizuri kuanza na mafunzo ya watu
wanaofanya tathmini katika maeneo ya kifundi na kiutawala.
Naye
Msimamizi wa Masuala ya Manunuzi katika Mradi wa Maboresho ya Mahakama, Bi.
Damasia Ndunguru, akizungumza pembeni mwa hafla hiyo ya ufunguzi, alieleza kuwa
mafunzo hayo yanayohusu ufanyaji wa tathmini za zabuni
yanajumuisha watumishi wa Mahakama kutoka kada mbalimbali.
“Mahakama
tumepokea zabuni 138, maana yake kuna washauri na wataalamu wa masuala ya
ujenzi sanifu na uzimamizi wa ujenzi wa miradi yetu tunayotarajia kuianza hivi
karibuni, ikiwemo ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki zaidi ya tisa na
Mahakama zingine 60 katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo,” alisema.
Amebainisha
kuwa kutoka kwenye maombi hayo 138 wanatarajia kupata Wazabuni 10 kwa ajili ya
kufanya kazi hiyo. “Timu hii iliyoteuliwa ipo hapa kupata mafunzo, uelewa na ujuzi
kabla ya kuanza zoezi hilo ili kuweza kwenda kwa haraka zaidi na ufanisi, hivyo
kukamilisha miradi yetu kwa viwango vinavyotakiwa,” alisema.
Mafunzo
hayo yanaendeshwa pia kwa kutumia Mkutano Mtandao kuunganisha watumishi wengine
waliopo katika kituo kingine cha Mahakama ya Wilaya Namtumbo ambao hawakuweza
kuhudhuria Arusha kutokana na majukumu mengine ya kimahakama.
Mahakama
ya Tanzania, kupitia Kitengo cha Maboresho, imeandaa mafunzo maalumu kwa
watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo Wahandisi, Wasanifu majengo, Maafisa
Ugavi, Mahakimu, Wasajili, Wahasibu, Wachumi na Watakwimu kuwajengea uwezo
katika masuala yanayohusu ufanyaji wa tathmini za zabuni.
Hatua
hiyo inafuatia baada ya kupata maombi kutoka kwenye makampuni ambayo yanataka
kutoa ushauri kuhusu masuala ya usanifu majengo pamoja na usimamizi wa miradi
ya ujenzi. Baada ya mafunzo hayo, timu hiyo itajichimbia kwa siku kadhaa
kufanya zoezi la tathmini kujua wazabuni wapi wanafaa kufanya kazi hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni