Na Faustine Kapama-Mahakama, Arusha
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka timu maalumu
iliyoundwa kuchambua maombi wa Wazabuni 138 kufanya jukumu hilo kwa kuzingatia
uadilifu na uzalendo wa hali ya juu na kuhakikisha kampuni zitakazopitishwa zina sifa ya kuweza kutekeleza miradi kwa ufanisi na kwa wakati .
Prof. Ole
Gabriel ametoa rai hiyo leo tarehe 3 Januari, 2023 alipokuwa anafungua mafunzo
ya siku tatu ambayo yamewaleta pamoja watumishi wenye kada mbalimbali wa Mahakama
ya Tanzania yanayofanyika katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini
hapa.
“Natamani
tujifunze kwenye mradi wa maboresho wa awamu ya kwanza kama tulifanya makosa
huko nyuma. Kosa ni kurudia kosa. Kuweni makini katika kupitia zabuni hizi.
Kuna maombi 138, lakini ni Wazabuni 10 tu ndiyo wanaotakiwa. Tunahitaji
Wakandarasi na Washauri wenye ubora, kwa hili nawataka muwe wazalendo kwa
maslahi ya Watanzania na mkizingatia thamani ya fedha,” alisema.
Amewataka
pia kuzingatia maslahi ya Mahakama, Serikali na umma wa Watanzania kwa ujumla
kwa kuzingatia kuwa Serikali imeridhia kuchukua mkopo mkubwa zaidi ili
kufanikisha ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vingine zaidi ya tisa,
ikiwemo kimoja ambacho kitajengwa Zanzibar, kazi ambayo ni kubwa na akashauri
utekelezaji wa miradi hiyo ifanyike kwa masaa 24 ili kumalizika kwa wakati.
“Tumepewa
fedha nyingi zaidi kuliko za mwanzo ambazo zilikuwa dola za Kimarekani milioni
65, hizi zilizokuja sasa ni dola za Kimarekani milioni 90, lakini muda ni
mfupi, tuna takribani miaka miwili tu, hivyo lazima tufanye kazi kwa kasi kubwa
na kwa ubora wa hali ya juu. Kutofaulu kwetu sisi sio chaguo letu na hatuweze
kurudi nyuma, tusonge mbele haraka na kwa usahihi,” alisema.
Kadhalika,
Mtendaji Mkuu amewahimiza watumishi hao kubadilika kifikira na kugeuza kuwa
fursa changamoto wanazokabiliana nazo wanapotekeleza majukumu yao. Amesema
hakuna changamoto ambayo haiwezi kuwa fursa, hivyo ni lazima wajijengee
utamaduni wa kuwa sehemu ya suluhisho, hasa kutatua changamoto walizonazo na
siyo kuwa mahiri katika kuzitolea taarifa.
“Mahakama
inafanya maboresho na mageuzi makubwa, tusingependa tuishie kwenye maboresho ya
majengo na mifumo ya TEHAMA. Maboresho makubwa na sahihi ni kwenye fikra zetu.
Hivyo ningetamani wote ambao mnashiriki hapa kujihakikishia nyinyi wenyewe
mnajiboresha kifikra, muwe watu wenye kubadilisha changamoto kuwa fursa na sio
kulalamika.,” alisema.
Prof. Ole
Gabriel amewaeleza watumishi hao kuwa anatamani Mahakama ya Tanzania ianze
mwaka kwa kasi nyingine, ikiwemo uboreshaji wa majengo, miundombinu na huduma
za Mahakama kwa lengo la kuharakisha huduma za utoaji haki kwa wananchi. Hivyo
akawahimiza kuchapa kazi kwa bidii na kujiepusha na uzembe, ubadhilifu na uvivu
wa aina yoyote mahali pakazi ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma.
“Hatujengi
kwa maana ya kuwa na majengo mengi mahakamani, bali tutengeneze mazingira ya
utoaji wa haki kwa Watanzania. Tunatamani Watanzania waone kuwa Mahakama
imekuwa bora zaidi kuliko miaka ya nyuma. Tunatamani mihimili mingine ione
kwamba yapo maboresho, wanayaona na tunataka wayaone zaidi na waje wajifunze.
Mahakama ni mahali patakatifu, hivyo lazima uadilifu na uzalendo uwe wa hali ya
juu kwa maafisa wa Mahakama na wasio maafisa wa Mahakama. Kwa hili, hakuna
lugha nyingine nyepesi ya kulielezea,” alisema.
Mahakama
ya Tanzania, kupitia Kitengo cha Maboresho, imeandaa mafunzo maalumu kwa
watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo Wahandisi, Wasanifu majengo, Maafisa
Ugavi, Mahakimu, Wasajili, Wahasibu, Wachumi na Watakwimu kuwajengea uwezo
katika masuala yanayohusu ufanyaji wa tathmini za zabuni.
Hatua hiyo
inafuatia baada ya kupata maombi kutoka kwenye makampuni ambayo yanataka kutoa ushauri
kuhusu masuala ya usanifu majengo pamoja na usimamizi wa miradi ya ujenzi.
Baada ya mafunzo hayo, timu hiyo itajichimbia kwa siku kadhaa kufanya zoezi la
tathmini kujua wazabuni wapi wanafaa kufanya kazi hizo.
Meza Kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu nyingine ya timu ya wataalam ya kuchambua zabuni (juu na chini) inayohudhuria mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni