Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 23 Januari, 2023
ametembelea mabanda ya maonesho ya utoaji wa elimu ya kisheria katika Viwanja
vya Nyerere Square jijini hapa na kusisitiza mambo matatu, ikiwemo wananchi
kuendelea kuuamini Mhimili wa Mahakama kama chombo pekee cha utoaji haki nchini.
Akizungumza na Waandishi
wa Habari kwenye viwanja hivyo katika siku ya pili ya Wiki ya Sheria baada ya
kutembelea madanda kadhaa, Prof. Ole Gabriel amewaambiwa wananchi kuwa uamuzi
wa kisheria unaotolewa na Mahakama haufanywi kiholela wala kuangalia utashi wa
mtu, bali hufuata sheria na ushahidi.
“Mwananchi anapaswa
kutambua kwamba pale anapofuatilia haki yake ni muhimu kwake kutoa ushahidi wa
kile anachoamaini kwamba ni haki yake. Anapokwepa kutoa ushahidi inakuwa ngumu kwa
uamuzi kufanyika,” amesema.
Amewaomba Watanzania
kuendelea kuilinda amani iliyopo nchini na kusisitiza kuwa haki ndiyo hasa
inayoleta amani, hivyo ni muhimu kuendelea kuuamini Mhimili wa Mahakama kwa
kuzingatia kuwa mtu anapokwazika kwenye mifumo ya kibiashara au yoyote ile huchagua
kwenye mahakamani kutafuta haki yake.
“Kwa hiyo tunawaomba
wananchi waendelee kuuamini Mhimili wa Mahakama kwamba unatenda haki na pale
ambapo kunaweza kuwepo na tashwishwi yoyote kwa baadhi ya watu, kwa sababu wale
wanaofanya kazi mahakamani ni binadamu, tunayo mifumo mizuri sana ya
kurekebishana ndani ya Mhimili,” amesema.
Akizungumzia suala la
maadili, Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa moja ya majukumu ya Tume ya Utumishi wa
Mahakama ni kufuatilia mienendo ya watumishi na kulinda taswila la Mhimili huo.
Akagusia pia uwepo wa Kamati za Maadili katika ngazi ya Mkoa na Wilaya ambapo Mkuu
wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya huwa ndiyo wenyeviti katika ngazi hizo.
Aidha, katika eneo la kiutawala,
Prof. Ole Gabriel ameeleza kuwa wamewekeza kwenye mafunzo kwa kada zote za
watumishi wakiwemo wadereva, makatibu mahsusi, watunza kumbukumbu na wengine ili
kuwaelewesha nini hasa Watanzania wanachokitarajia kutoka kwao katika suala
zima la utoaji haki.
“Tumewekeza zaidi katika
kuwaelimisha na kuwaelewesha umuhimu wa maadili ndani ya Mahakama kwa sababu Mahakama
ni eneo takatifu, hii itawezesha kutekeleza ile nguzo ya tatu ya mpango mkakati
kuhusu kuimarisha imani kwa wadau.
Tumejipanga kuhakikisha wananchi
wanapata haki kwa wakati, kwa uwazi na bila tashwishwi zozote za rushwa,” amesema.
Mtendaji Mkuu ametumia
fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa
na Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwezeshaji mkubwa ambao umechochea uboreshaji
wa miundombinu mbalimbali ya Mahakama ikiwemo ujenzi wa majengo ya kisasa.
“Mahakama hatufanyi
biashara, hatuuzi haki, hatuuzi magari, mahindi wala ng’ombe, sisi tunatoa
haki. Kwa hiyo miundombinu yetu inategemea uwezeshwaji kutoka serikalini. Mimi
kama Afisa Masuhuli lazima nitoe shukrani kwa Serikali, kwa kweli tunawezeshwa
vizuri, tunatumia fedha hizo vizuri na matokeo yanaonekana. Bila uwezeshwaji
huo tungekuwa na changamoto kubwa zaidi,” amesema.
Prof. Ole Gabriel akabainisha
pia kuwa ujenzi wa Mahakama katika ngazi mbalimbali kama Mahakama za Mwanzo
unaendelea kwa kazi kubwa, ambapo Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita
vimeshajengwa mpaka sasa na vingine 12 vitajengwa kufika mwaka 2024, lengo ni
kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi.
Mtendaji Mkuu aliwasili
katika Viwanja vya Nyerere Square majira ya saa tatu asubuhi na kutembelea
madanda ya maonesho kadhaa ambayo yameandaliwa na wadau mbalimbali wa Mahakama
wakiwemo Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Bandari, Mkemia Mkuu wa
Serikali, Chuo Kikuu cha Dodoma, Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa ya
Kulevya, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Akiwa katika mabanda hayo,
Prof. Ole Gabriel alipata maelezo namna taasisi hizo zinavyofanya kazi kutoka
kwa watendaji mbalimbali. Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu alipata fursa ya
kuuliza maswali ili kupata ufafanuzi wa hoja mbalimbali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni