Jumatatu, 23 Januari 2023

WANANCHI WAMIMINIKA NYERERE SQUARE KUPATA HUDUMA ZA KISHERIA

Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma

Watanzania mkoani Dodoma na maeneo ya jirani leo tarehe 23 Januari, 2023 wameendelea kujitokeza katika Viwanja vya Nyerere Square kupata elimu na ufafanuzi wa kisheria kwenye masuala kadhaa kutoka kwa watumishi na wadau mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.

Katika siku ya pili ya Wiki ya Sheria, wananchi wamejitokeza kwa wingi kutembelea mabanda ya Mahakama, wadau wake na ofisi zingine za Serikali, wakiwemo Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kama picha hapa chini zinavyoonyesha.

Banda la Kituo cha Usuluhishi limeonekana kutembelewa na watu wengi ambao wameonyesha shauku ya kupata maelezo zaidi kuhusu njia hiyo bora ya kutatua migogoro ambayo ina faida nyingi, ikiwemo kumalizika kwa mashauri kwa haraka na kwa gharama nafuu, huku wadaawa wakitoka mahakamani wakiwa wameshikana mikono.

Kadhalika, wananchi walionekana wengi katika banda la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu vizazi na vifo, utaratibu wa kupata cheti cha kuzaliwa na mambo mengine ya kifamilia.

Wananchi wakipata maelezo kutoka kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Wanjah Hamza (wa tatu kushoto) kuhusu faida za kutumia njia ya usuluhishi katika kutatua migogoro mbalimbali.
Wananchi (kulia) wakiwa katika banda la Mahakama linaloshughulikia masuala ya Mirathi.


Sehemu ya wananchi wakiwa kwenye banda la Kurugenzi ya Uendeshaji wa Mashauri.
Wananchi wakipata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kutoka kwa ofisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Mwananchi (kulia) akipokea fomu maalumu kutoka kwa afisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
Mwananchi akijadili jambo baada ya kupata maelezo kuhusu masuala ya ardhi alipokuwa kwenye banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Ofisa kutoka Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamini (wa pili kushoto) akifafanua jambo kwa wananchi waliotembelea banda lao.
Wananchi wakipata maelezo kutoka kwa watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).
Mwananchi akipata huduma za kisheria katika banda la Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).
Kwaya ya Mahakama ya Tanzania (juu na chini) nayo haikuwa nyuma kutembelea mabanda yaliyoandaliwa na Mahakama na wadau mbalimbali. 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni