·Jaji Mkuu aainisha mambo sita muhimu yanayohitaji kuzingatiwa
Na Faustine Kapama-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 17 Februari, 2023 amezindua Baraza la Wafanyakazi
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na kusisitiza mambo sita kwa wajumbe, ikiwemo
kuzingatia maadili na kutunza siri za ofisi, ambayo yanahitaji kuzingatiwa wanapotekeleza
majukumu yao ya kikatiba.
Uzinduzi huo umefanyika
katika ofisi ndogo za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Tume ya Utumishi wa Mahakama,
akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Baraza hilo, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Mhe. Prof. Juma amesema kwa kuzingatia majukumu ya Tume ya Utumishi wa
Mahakama ambayo yametajwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4, 2011,
watumishi hao wanatakiwa kujituma na kuwa na uwajibikaji wenye tija wakati wa utoaji
haki.
Jaji Mkuu pia amesisitiza
Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuzingatia kuwa Mahakama
ya Tanzania imefanya maboresho ya makusudi kutoka kutumia TEHAMA katika kusambazia
taarifa au habari mpaka kuifanya nyenzo muhimu kwenye utendaji kazi wa kila
siku wa Mahakama.
“Maboresho yanayoendelea
ndani ya Mahakama yawe chachu kwa Sekreterieti ya Tume kuwezesha kazi zake na
za Tume ziweze kutumia TEHAMA katika shughuli zao za kila siku, mfano utunzaji
wa kumbukumbu na taarifa na kwenye mikutano ya Tume na Kamati zake ili zipunguze na
kuondoa kabisa matumizi ya karatasi,” amesisitiza.
Aidha, Jaji Mkuu amewahimiza
watumishi wa Sekreterieti kuwa wabunifu (creativity, innovative) katika
kazi zao za kuiwezesha Tume ya Utumishi kutimiza wajibu wake wa kikatiba na kisheria.
Amesema ubunifu ni lazima ujengwe kutokana na misingi imara ya uelewa wa kina
wa vifungu vya Katiba, sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayoongoza
Tume ya Utumishi wa Mahakama.
“Ubunifu unaongezwa kwa
kujisomea, kujitafutia taarifa na kujiboresha kwa kujifunza kutoka Tume zingine
za Mahakama zenye viwango vya ubora,” Mhe. Prof. Juma amebainisha. Kadhalika,
Jaji Mkuu alisisitiza suala la maadili mema.
Amesema Tume ya Utumishi
wa Mahakama imepewa jukumu la kikatiba la kusimamia maadili na nidhamu, hivyo wafanyakazi
wa Sekreterieti ya Tume wanatakiwa kuwa na maadili yasiyotiliwa shaka. Jaji
Mkuu amesema itakuwa kichekesho kwa Tume kuhubiri maadili huku watumishi katika
Sekretarieti wakikosa uadilifu wanapotekeleza majukumu yao.
Jambo jingine ambalo
Mhe. Prof. Juma amesisitiza linahusu utunzaji wa siri za ofisi. Amesema Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na.
4/2011 imesheheni vifungu kadhaa ambavyo vinasisitiza umuhimu wa kutunza siri za
ofisi.
“Kifungu cha 16 (1) cha
Sheria hii, kinahusu wajibu wa Makamishna, Katibu na Naibu Katibu kuapa mbele
ya Mwenyekiti kabla ya kuanza shughuli za Tume. Kifungu kidogo cha (2) kimempa
Mwenyekiti mamlaka ya kumtaka mtumishi yoyote katika Sekreterieti ya Tume, kula
kiapo kwa mujibu wa Jedwali la Tatu la Sheria Na. 4/2011,” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha
kuwa msisitizo wa vifungu vya sheria ni kumbusho kwa watumishi kuwa ni kinyume
cha sheria kwa mtumishi wa Tume kutoa taarifa yoyote ya Tume kwa mtu
asiyehusika bila kibali ama kuzingatia taratibu. Aidha, aliweka mkazo katika
suala zima la utii wa kazi, kwa viongozi na pia kuheshimiana.
“Haya yote yakizingatiwa
utendaji utakuwa wenye tija. Chukueni
tahadhari zote kila wakati kwa kuwa ndugu, majirani na marafiki watakaposikia
kuwa wewe upo Sekretarieti ya Tume watakutafuta ili uwashauri. Epukeni mtego
huo kwa kuwa kufanya hivyo ni ukiukaji wa maadili. Kwa muktadha huo, upo
umuhimu wa viapo kushushwa kwa watumishi wote wa Sekretarieti,” amesema.
Awali akimkaribisha kuzindua
Baraza hilo, Prof. Ole Gabriel alimweleza Jaji Mkuu kuwa katika kutekeleza majukumu
yao ya kila siku, watumishi wa Sekretarieti ya Tume huongozwa na Dira ya Tume
ambayo ni kuwa kitovu cha ubora katika kusimamia watumishi wa Mahakama Tanzania
Bara. Aidha, alisema watumishi hao wanaongozwa na Dhima ya Tume ambayo ni
utoaji endelevu wa huduma ya ushauri na usimamizi wa rasilimali watu katika
utumishi wa Mahakama Tanzania Bara.
Mtendaji Mkuu alieleza
pia kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Sekretarieti ya Tume imejiwekea malengo
ambayo yatasaidia kufanikisha majukumu yake, ikiwemo uwezeshaji wa maadili
katika Mahakama ya Tanzania unaboreshwa na kuimarisha huduma za utawala bora
katika Tume ya Utumishi wa Mahakama.
“Kwa hiyo, kimsingi
tunajitahidi kuhakikisha kuwa utawala bora unakuwepo na pia mpango mkakati wa
kuzuia rushwa unatekelezwa kwa ufanisi. Kama mnavyofahamu katika shughuli za
watumishi wa Mahakama masuala ya maadili na kupambana na rushwa ni jambo la
msingi sana,” alisema.
Prof. Ole Gabriel alieleza pia kuwa katika kipindi cha Julai 2022 hadi Disemba 2022 Sekretarieti ya Tume imefanikiwa kutekeleza majukukumu yake, ikiwemo kuwezesha Tume kufanya vikao vitatu na katika masuala mbalimbali kama uteuzi wa Majaji 22 wa Mahakama Kuu na Msajili wa Mahakama ya Rufani, kuthibishwa kwenye uongozi na ajira katika masharti ya kudumu kwa baadhi ya watumishi na kusimamia nidhamu na maadili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni