Na Christopher Msagati-Mahakama, Manyara
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza leo tarehe 17 Februari,
2023 amekutana kwa mara ya kwanza na viongozi wa Mahakama Mkoa wa Manyara kujadili
mambo mbalimbali ya kiutendaji.
Akizungumza katika kikao kazi
hicho, Mhe. Kahyoza alisisitiza watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano na kuzingatia
nidhamu ili kufanikisha malengo ya Kanda na kuboresha huduma za utoaji haki kwa
wananchi.
Jaji Mfawidhi huyo alisema
kuwa ni jukumu la viongozi wote kusimamia masijala zao kwa ufasaha, ikiwemo vielelezo
vyote vinavyofikishwa mahakamani kila siku.
Viongozi hao walitumia
nafasi hiyo kupitia na kujadili maoteo ya bajeti ya Mahakama Mkoa wa Manyara na
Wilaya zake kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Kadhalika, walitumia kikao
hicho kufahamiana kwa vile ni mara ya kwanza kwa viongozi hao kukutana tangu
kuanzishwa kwa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara mwezi Novemba, 2022.
Kikao hicho kilichofanyika
majira ya asubuhi katika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Manyara kimehudhuriwa na
Jaji wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Gladys Barthy, Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu, Mhe. Bernard Mpepo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Manyara, Mhe. Mariam Lusewa pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Manyara, Bw. Jacob
Swalle.
Viongozi wengine
waliokuwepo ni pamoja na Mahakimu Wakazi Wafawidhi, Maafisa Utumishi na Tawala wa
Wilaya za Babati, Hanang, Mbulu, Kiteto na Simanjiro katika Mkoa wa Manyara.
Wajumbe wa kikao wakifuatilia uwasilishaji wa maoteo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 katika kikao kazi hicho.
(Habari
hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama Dar es Salaam).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni