·Jaji Mfawidhi aonya matumizi ya ofisi mtandao kutokwamishwa
Na. Francisca Swai-Mahakama, Musoma.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya
amewapongeza viongozi wa Mahakama kwa utendaji kazi mzuri unaoridhisha.
Mhe.
Mtulya ametoa pongezi hizo hivi karibuni katika kikao cha menejimenti cha Mahakama katika Kanda hiyo
kilichofanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama mpya ya Wilaya Rorya.
Jaji
Mfawidhi huyo amesisitiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
hasa wakati huu ambapo Mahakama zote za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya
zinaelekea kuanza matumizi ya ofisi mtandao.
Ameelekeza
Mahakama zote kuwa na mfumo wa Key Word Classification na
kuuzingatia ili kutokwamisha matumizi ya ofisi mtandao pale yatakapoanza kwani uongozi
wa Kanda hautomvumilia mtumishi yeyote atakayekuwa kikwazo.
Katika
kikao kazi hicho ilifanyika pia tathmini ya maadhimisho ya Wiki na Siku ya
Sheria nchini kwa mwaka 2023 ambapo Mhe. Mtulya alionyesha kuridhishwa jinsi
watumishi wa kada mbalimbali walivyoshiriki.
“Nimeridhishwa
sana na namna watumishi wote walivyojitolea kwa hali na mali kufanikisha
maadhimisho hayo, hii ni ishara nzuri ya umoja (team work),” alisema.
Kadhalika,
amewapongeza watumishi hao kwa kuonyesha upendo kwa jamii, kuwajali na
kuwafikia watu wenye mahitaji maalumu katika Wiki ya Sheria.
Akiongea
katika kikao hicho, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Frank
Moshi alisisitiza kila Mahakama ndani ya Kanda hiyo kuhakikisha inamaliza
mashauri yake kwa wakati na kutozalisha mashauri ya mlundikano (backlog).
Naye
Mtendaji wa Mahakama katika Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya aliwasilisha
taarifa kuhusu ukarabati wa Mahakama ya Mwanzo Kenkombyo iliyoko katika Wilaya
ya Bunda.
Katika
kikao hicho wajumbe walionesha kuridhishwa na taarifa hiyo. Bw. Chonya pia alisisitiza
katika taarifa yake kuhusu upandaji miti na uwekaji wa vigingi katika viwanja vya
Mahakama ili kulinda mipaka ya maeneo hayo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni