Jumatatu, 20 Februari 2023

WANAFUNZI BISHOP HILHORST SEKONDARI WATEMBELEA KITUO JUMUISHI MOROGORO

Na. Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro 

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bishop Hilhorst iliyopo mjini hapa hivi karibuni walitembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro ili kujifunza mambo mbalimbali, ikiwemo kujua namna kinavyofanya kazi ya kuwahudumia wananchi. 

Wanafunzi hao ambao walikuwa na shauku ya kujua namna Vituo hivyo vipya kwa Tanzania na Afrika vinavyoendesha huduma zake, walipokelewa na Mwenyekiti wa Elimu na Msaidizi wa Jaji, Mhe. Lameck Mwamkoa. 

Akiongea na wananfunzi hao, Mhe. Mwamkoa aliwafundisha masuala mbalimbali, ikiwemo Muundo wa Mahakama, Haki za Mtoto na namna Mahakama inavyoshirikiana na wadau katika mnyororo wa utoaji haki. 

Alieleza kuwa Kituo Jumuishi ni msaada mkubwa kwani mwananchi huweza kupata huduma za kisheria karibu zote katika jengo moja, hivyo kumrahisishia kupata haki. Amesema uwepo wake umeongeza ushirikiano toka kwa wadau wa haki. 

Aidha, Mhe. Mwamkoa aliwaeleza wanafunzi hao kuwa Mahakama inatoa elimu ya ulinzi kwa mtoto ili kuwalinda, hivyo akawaasa kutoa taarifa sehemu husika pale wanapokuwa wametendewa mambo yasiyostahili ikiwemo kunyanyaswa kingono. 

Kwa upande wake, Mwanafunzi Betha Michael alitoa shukurani kwa niaba ya wenzake kwa Mahakama Kanda ya Morogoro kwa kuwapatia nafasi hiyo adhimu ya kujifunza kwani wameongeza elimu itakayowasaidia. 

“Kabla ya kuja hapa nilikuwa naogopa kufika mahakamani, ila sasa nimepata elimu kuwa Mahakama ni rafiki yetu mzuri na yupo kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapatiwa haki zao,” alieleza. 

Katika ziara yao, wanafunzi hao walipata nafasi ya kuhudhulia kikao kimoja cha Mahakama ambacho kilikuwa kinasikiliza kesi ya mauaji (murder session) kilichoendeshwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabriel Malata. 

Kuanzishwa kwa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro siyo tu kimerahisisha utoaji haki katika Kanda hiyo, bali pia kimekuwa kivutio kikubwa kwa Vyuo na Shule ambapo wanafunzi wamekuwa wakibisha hodi mara kwa mara ili kujifunza namna kinavyotekeleza majukumu yake. 

Mwenyekiti wa Elimu na Msaidizi wa Jaji, Mhe. Lameck Mwamkoa akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bishop Hilhorst walipotembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro hivi karibuni.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bishop Hilhorst wakifuatilia elimu inayotolewa wakati walipotembelea Kituo hicho.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bishop Hilhorst wakiwa katika picha ya pamoja na walimu wao na Mwenyekiti wa Elimu na Msaidizi wa Jaji, Mhe. Lameck Mwamkoa.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni