Jumatatu, 20 Februari 2023

MAHAKAMA KIGOMA YAWEKA MIKAKATI KUMALIZA MASHAURI, KURAHISISHA UTENDAJI

Na. Aidan Robert-Mahakama, Kigoma.

Mahakama ya Tanzania Kanda ya Kigoma hivi karibuni ilifanya kikao cha Kamati ya Uongozi kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji na kiutawala, ikiwemo kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha huduma za haki zinatolewa kwa wananchi kwa wakati.

Akizungumza wakati anafungua kikao hicho cha kwanza kwa mwaka 2023, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha aliwataka wajumbe wa Kamati hiyo kuweka mikakati itakayosaidia kuongeza kasi ya umalizaji wa mashauri na kurahisisha shughuli za kiutawala.

Jaji Mfawidhi huyo amesisitiza kuwa usuluhishi utumike ipasavyo kama njia mbadala ya kutatua migogoro, hasa ile yenye asili ya madai na kuhimiza kasi ya matumizi ya Mahakama Mtandao katika kuratibu shughuli mbalimbali za kiutawala ili kurahisha utendaji na kuongeza ufanisi.

“Mtakumbuka tarehe 1 Februari, 2023 wakati natoa hotuba yangu katika maadhimisho ya Siku ya Sheria niliujulisha umma kwamba kwa mwaka 2022, Kanda nzima iliweza kumaliza kwa njia ya usuluhishi mashauri 256 kati ya 5,366 yaliyosajiliwa, sawa na asilimia 4.8,” alisema.

Hivyo alisisitiza kwa mwaka 2023 lazima Kanda hiyo iwekeze zaidi katika eneo hilo pamoja na kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa njia mbalimbali kupitia vipindi vya Radio ili wananchi wengi wajue umuhimu na faida za utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhuishi.

Naye Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Stephen Magoiga, akizungumza katika kikao hicho aliwataka wajumbe kwenda kusimamia vigezo vya ukaguzi wa Mahakama na Magereza, hususani suala la ujazaji sahihi wa rejesta na uzingatiaji wa taratibu zote katika usikilizaji wa mashauri.

Aliwahimiza kufanyia kazi changamoto na mapungufu yaliyobainishwa katika ukaguzi wa Mahakama na Magereza katika kipindi cha robo mwaka kati ya Oktoba hadi Disemba, 2022.

Mambo mbalimbali yalijadiliwa na kuwekewa mikakati ya utekelezaji katika kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma na kuwashirikisha wajumbe kutoka Makao Makuu ya Kanda, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya sita.

Miongoni mwa masuala hayo ni ongezeko la kasi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kusajili, usikilizaji na usimamizi wa shughuli za mashauri na kiutawala.

Masuala mengine ni tathmini ya utekelezaji wa bajeti kwa robo mwaka ya Oktoba hadi Disemba, 2022, mapitio ya taarifa ya Mkaguzi wa Ndani na tathmini ya uendeshaji wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka 2023.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (kulia) akifuatilia kwa karibu yaliyokuwa yakiendelea kwenye kikao kazi cha Kamati ya Uongozi cha Mahakama, Kanda ya Kigoma. Kulia kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Stephen Magoiga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (katikati) akichukua kumbukumbu mbalimbali wakati wa kikao cha Kamati ya Uongozi. Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Stephan Magoiga(kushoto) na Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka.
Viongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma wakiwa kwenye kikao hicho. Kutoka kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadieli Mariki, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa  na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama mpya ya Wilaya Buhigwe, Mhe. Venance Katoke.
Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka (aliyesimama) akifafanua jambo wakati wa kikao hicho alipokuwa anawasilisha taarifa ya utendaji.

Wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma wakiendelea na kikao.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni