Jumanne, 21 Februari 2023

MAHAKAMA MOROGORO KUSHIRIKIANA NA TANAPA KULINDA HIFADHI

Na. Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe ameahidi kutoa ushirikiano kwa Hifadhi za Taifa (TANAPA) ili kuhakikisha hifadhi za wanyama pori zinalindwa kwa vizazi vilivyopo na vinavyokuja. 

Mhe. Ngwembe alitoa ahadi hiyo hivi karibuni alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kufuatia mwaliko toka kwa Mkuu wa Hifadhi wa TANAPA, Kanda ya Morogoro ili kuona na kujifunza namna wanavyoendesha shughuli za uhifadhi. 

Alisema Mahakama Kanda ya Morogoro itasimamia katika kutenda haki. “Hatutamuonea mtu wala kumfaidisha mtu, sisi tutasimamia katika kutafsiri sheria ili pande zote zipate haki yao inayostahili,” alisema Mhe. Ngwembe. 

Jaji Mfawidhi huyo alisema fulsa waliyoipata ya kutembelea hifadhi hiyo imewapa uwezo wa kuona na kujifunza mambo mbalimbali, jambo ambalo litawarahisishia  katika utendaji wa kazi. 

Aliongeza kuwa TANAPA na Mahakama zina mahusiano mazuri ya muda mrefu ukizingatia viongozi walishawahi kufika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro kutoa elimu kwa wadau wa Mahakama ili kupunguza makosa ya ujangili. 

Naye Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwepo kwenye ziara hiyo alisisitiza kuwekwa mipaka kati ya hifadhi na vijiji ili kuondoa migogoro. 

Awali, akisoma taarifa fupi ya hifadhi kwa niaba ya Kamishna wa Hifadhi, Afisa Mwandamizi wa Hifadhi Apaikunda Mungure aliishukuru Mahakama kwa hatua inazochukua, ikiwemo kusikiliza kesi na kutolea hukumu kwenye ngazi ya vijiji kwani imekuwa ikipeleka Hakimu mpaka eneo la tukio ili kusikiliza kesi hizo. 

“Inapotokea mifugo imekamatwa hifadhini hupelekea askari wa hifadhi kusitisha majukumu mengine na kuanza kuichunga mpaka maamuzi yatakapokamilika. Hivyo kitendo cha kuzipa kipaumbele kesi zetu itaturahisishia uwajibikaji,” alisema.

Wengine walioshiriki ziara hiyo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kanda hiyo, Mhe. Augustina Mmbando, baadhi ya Mahakimu pamoja na wawakilishi kwa kila kada miongoni mwa watumishi wa Mahakama kutoka Kanda ya Morogoro.

Msafara huo wa Mahakama ulipata pia nafasi ya kutembelea mradi wa kufua umeme katika Bwawa la Mwalimu Nyerere na kujionea namna shughuli za ujenzi na ujazaji maji unavyoendelea.

Ukiwa katika bwawa hilo, Msafara huo ulipokea taarifa fupi kutoka kwa Mkandarasi Mkazi Lutengano Mwandambo ambaye alieleza kuwa mradi huo umefikia asilimia 81.8 na shughuli ya ujazaji maji inatarajiwa kukamilika ndani ya misimu miwili au mitatu endapo mvua zitanyesha kwa wastani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (wa tano kulia) pamoja na watumishi wengine wakiwa katika lango la kuingilia kwenye Hifadhi ya Nyerere. Viongozi wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba (wa pili kushoto) na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Augustina Mmbando (wa tatu kushoto).
Msafara kuingia hifadhini unaendelea.

Sehemu ya wanyama (juu Simba na chini Tembo) wanaopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.

Muongoza watalii akitoa elimu kwa msafara wa Mahakama wakati ulipofika kwenye moja wapo ya mito iliyomo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (wa pili kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Messe Chaba (wa kwanza kushoto), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Augustina Mmbando (wa nne kushoto) na watumishi wengine wakipata maelekezo toka kwa afisa wa TANAPA.
Msafara ukiwa mbele ya ofisi za Hifadhi ya Taifa Nyerere.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wahifadhi toka TANAPA mbele ya mti wa kihistoria unaopatikana ndani ya hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Mti huo unakadiliwa kuwa na miaka zaidi ya 1,500.
 

Mkandalasi Mkazi Lutengano Mwandambo (aliyevaa suruali ya bluu) akitoa maelezo kwa msafara wa Mahakama ulipotembelea mradi wa bwawa la kufua umeme la Mwl. Nyerere.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni