Jumatano, 15 Februari 2023

MASHAURI 17 YA JINAI KUSHUGHULIKIWA NDANI YA MWEZI MMOJA

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma imepanga kushughulikia mashauri yanayohusu mauaji 17 katika kipindi cha mwezi mmoja.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Silivia Lushasi amesema mashauri hayo yatasikilizwa na Majaji wawili kwenye vikao maalumu (sessions) vinavyofanyika mkoani Singida.

Majaji hao kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma ni Mhe. Suleiman Hassan ambaye atasikiliza mashauri tisa kuanzia tarehe 13 Februari, 2023 hadi tarehe 28 Februari, 2023.

Jaji mwingine ni Mhe. Fatma Khalfan ambaye atasikiliza mashauri nane na ataanza jukumu hilo tarehe 1 Machi, 2023 hadi tarehe 16 Machi, 2023.

“Sambamba na taarifa hii, Mkoa wa Singida una mashauri 16 ambayo yanasubiri kusikilizwa (uncauselisted) ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi kuna mashauri 10, Iramba manne na Manyoni mawili,” Naibu Msajili huyo alisema.

Mhe. Lushasi alibainisha kuwa idadi hiyo ya mashauri tajwa haihusishi mashauri yanayosubiri washitakiwa kusomewa kwa mara ya kwanza (plea taking). Katika kikao hicho wadau wameahidi kutoa ushirikiano mkubwa na wamejipanga vizuri ili kuhakikisha mashauri hayo yanamalizika.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Seleiman Hassan ambaye ni miongoni mwa Majaji wanaosikiliza mashauri hayo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Silivia Lushasi akitoa ufafanuzi wa jambo fulani katika kikao hicho.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Bw. Sumera Manoti akieleza jambo.

Sehemu ya wajumbe wa kikao  wakifuatilia kwa umakini mjadala.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni