Jumanne, 14 Februari 2023

UJUMBE WA BENKI YA DUNIA, WATAALAMU WA MAHAKAMA WAKUTANA MWANZA

Na Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza 

Ujumbe wa Benki ya Dunia leo tarehe 14 Februari, 2023 umekutana na wataalam wa Mahakama ya Tanzania ili kupitia taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uboreshaji wa huduma za kimahakama inayofadhiliwa na taasisi hiyo ya kifedha. 

Akiukaribisha ujumbe huo, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Angelo Rumisha aliwashukuru wote kwa kuweza kufika kwenye kikao maalumu cha siku tatu kinachofanyika kwenye ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza. 

Kwa upande wake, Mbobezi Mwandamizi wa Asasi za Umma kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owour ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuweza kuonyesha ushirikiano katika miradi mbalimbali ya ujenzi ambayo Benki ya Dunia imekuwa ikiifadhili. 

“Tumekuja katika kipindi hiki kwa ajili ya kuangalia utekelezaji na mwendelezo wa miradi hii na kuona mikakati ya uendelezaji iliyopo kwa sasa, jinsi tulivyofanikiwa kufikia malengo na maboresho tunayotazamia,” alisema. 

Nae Mbobezi wa Asasi za Umma kutoka Benki ya Dunia, Bi Clara Maghani alionyesha furaha yake kwa matunda yaliyopatikana, ikiwemo ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) ambacho walibuni kwa pamoja na timu ya wataalamu wa Mahakama. 

“Tunataka kile ambacho tulibuni hapo awali hata kwa miaka mitano ijayo kinafikia malengo. Tunaka kila sehemu ambayo tulibuni IJC ifanye kazi jinsi ilivyotarajiwa. Katika kikao hiki tunategemea kujadili mipango ijayo ya maboresho ya Mahakama kwa manufaa zaidi ya wananchi,” alisema. 

Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel. 

Mhe. Chuma aliwaambia wageni kutoka Benki ya Dunia kuwa Mahakama imekuwa ikifanya vizuri katika miradi yote ambayo imeshatekelezwa na inayoendelea kwa sasa, hivyo akaipongeza timu nzima ya maboresho kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. 

Kwa upande wake, Prof. Ole Gabriel aliwaomba wajumbe wa kikao hicho kuja na sura ya Mahakama bora ijayo kupitia maboresho mbalimbali yatakayofanyika.

Katika kikao hicho, wakuu wa vitengo watawasilisha taarifa zao za utendaji kazi ikwemo mafanikio, changamoto na matarajio wanayotegemea kuyafikia ili kwenda na azma ya Benki ya Dunia katika kufikia malengo mbalimbali ndani ya Mahakama.

Mbobezi Mwandamizi wa Asasi za Umma kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owour akieleza jambo wakati wa kikao kilichofanyika leo tarehe 14 Febriari, 2023 katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbad Chuma akizungumza kwenye kikao hicho.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akieleza jambo kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Angelo Rumisha akifafanua jambo alipokuwa anaongea kwenye kikao hicho.

Wajumbe wa kikao hicho wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya ufunguzi.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni