·Ahimiza mabadiliko kifikra kuongeza ufanisi, uwazi, ubora wa huduma za utoaji haki
Na Faustine Kapama-Mahakama, Zanzibar
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 13 Februari, 2023 ameungana na
wananchi wa Zanzibar, akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuadhimisha Siku ya Sheria visiwani humo na
kuhimiza mabadiliko ya kifikra kuelekea haki mtandao ili kuongeza ufanisi,
uwazi na ubora wakati wa kutoa huduma za haki.
Akizungumza wakati wa
maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Mahakama Kuu Zanzibar, Mhe.
Prof. Juma amesema kuwa kauli mbiu ya Siku ya Sheria inayohusu “Haki Mtandao
kwa Kukuza Uchumi na Ustawi wa Jamii” ni ahadi ambayo Jaji Mkuu wa Zanzibar
anaitoa kwa Rais, wananchi na wadau wote wa sekta ya sheria Zanzibar kuwa
wamejipanga kufanya mabadiliko katika utoaji wa haki.
“Kama tunavyoelewa,
ahadi siku zote ni deni na ninaamini kupitia maadhimisho haya tutapata sisi
faida ya ufanisi, uwazi na ubora ambao siyo tu utasaidia utoaji wa haki lakini
pia utasaidia uchumi na jamii ya watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa ujumla,” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha
kuwa kwa kawaida mageuzi makubwa kama yanayoahidiwa huleta mabadiliko siyo
kutokana na uwezeshaji ambao Rais wa Zanzibar ameahidi kwamba ataiwezesha
Mahakama ili ifikie ahadi hiyo, lakini yanahitajika mabadiliko ya kifikra, kimtanzamo
na namna huduma za haki zinavyotolewa.
“Tunapozungumzia mabadiliko
ya kifikra ni ile ‘business process’,
tumezoea ule utaratibu wa kawaida wa kimahakama, shauri linaanzia hatua fulani
na kupitia milolongo mingi, lakini mabadiliko ya fikra, ile ‘business process’ ya Mahakama tunatakiwa kuiangalia upya. Kwa hiyo,
katika utoaji wa haki tunahitaji kutoka katika zile fikra za kizamani na kuja katika
fikra mpya,” Mhe. Prof. Juma alisisitiza.
Aliwakumbusha wananchi maneno
aliyosema Rais Mwinyi mwaka jana katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria Dodoma ambapo
aliwafahamisha azma ya Serikali yake ya kujenga uchumi wa bluu na kueleza kuwa ili
kufanikiwa lazima kuwepo mfumo wa kisheria na kimahakama ambao unaendana na
uchumi huo.
“Kwa hiyo, maana yake ni
kwamba ahadi mnayotoa leo yeye tayari yupo tayari kufanikisha, itabaki sisi na
fikra zetu ili mfumo wetu wa sheria uweze kutoa huduma katika huo uchumi wa
bluu,” aliwaeleza wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo.
Baada ya kuwasilisha
salamu hizo, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla alimkaribisha Rais
Mwinyi kuzindua Bendera na Nembo ya Mahakama ya Zanzibar. Kadhalika, Jaji Mkuu
huyo alimkabidhi Rais Mwinyi ripoti ya utendaji ya Mahakama ya Zanzibar kwa
mwaka 2022 kabla ya kumkaribisha kuongea na wananchi.
Akiongea na taifa kupitia maadhimisho hayo, Mhe.
Dkt. Mwinyi amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama
Zanzibar. Amesema kitendo ya Jaji Mkuu wa Tanzania na ujumbe wake kufika Zanzibar
na kuhudhuria maadhimisho hayo ni dalili tosha za kuimarika kwa ushirikiano
huo.
Kadhalika, Rais Mwinyi
ameipongeza Mahakama ya Zanzibar kwa kuja na kauli mbiu hiyo ambayo inaenda
sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa kuhusu Serikali Mtandao. Amesema kuwa
umefika wakati wa kufanya mageuzi makubwa katika mfumo wa utoaji haki nchini
kwa vile utaratibu wa kuendesha mashauri kwa kutumia makaratasi umepitwa na
muda.
Amesema anatambua kuwa
haki mtandao lazima iende sambamba na uwepo wa mambo mbalimbali, ikiwemo ujenzi
wa majengo ya kisasa kwa taasisi za haki, hususani Mahakama, uwepo wa nyenzo za
TEHAMA, kuwajengea uwezo watumishi kuhusiana na matumizi ya teknolojia na
kuwajengea uwezo mkubwa maafisa TEHAMA ili waweze kuanzisha na kusimamia mifumo
pamoja na usalama wa miundombinu hiyo.
“Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar itaendeleza juhudi ambazo zimeanzishwa za kuimarisha taasisi zetu
za haki ili ziweze kufanya kazi zake kwa ufanisi. Serikali pia itahakikisha kwamba
inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuboresha miundombinu muhimu ya taasisi
hizo ili iende sambamba na mifumo ya haki mtandao ambayo tunaendelea kuianzisha,”
alisema.
Rais Mwinyi amebainisha
kuwa matumizi ya TEHAMA yanafaida nyingi katika shughuli za utoaji haki,
ikiwemo usikilizaji na uamuzi wa mashauri kwa haraka, upatikanaji wa takwimu
sahihi za mashauri kwa taasisi za sheria na ufuatiliaji bora na usimamizi mzuri
wa mashauri.
Amesema kupitia haki
mtandao hakutakuwa na ulazima kwa Majaji wa Mahakama Kuu kusafiri kwenda Pemba
kusikiliza mashauri, kwani mashauri hayo yataweza kusikilizwa na kuamriwa kwa
mfumo wa TEHAMA, shahidi hatalazimika kufika kwenye jengo la Mahakama kutoa
ushahidi, bali inaweza kuandaliwa mifumo na kuweza kutoa ushahidi wake hata kwa
kutumia simu yake ya mkononi.
“Kwa utaratibu huo mienendo
ya kesi itapatikana kwa haraka kwa wahitaji. Zaidi ya hayo watumishi wa taasisi
za haki wataweza kufanya mikutano yao, kubadilishana uzoefu hata kushiriki mafunzo
kwa njia ya mtandao bila kulazimika kusafiri au kuondoka kwenye ofisi zao. Hayo
yakifanyika tutaokoa fedha nyingi ambazo Serikali hutumia kugharamia shughuli
hizo, badala yake fedha hizo zitaelekezwa kwenye shughuli nyingine za
maendeleao ya nchi,” Rais Mwinyi amesema.
Kwa upande wa Mawakili na
wananchi, Mhe. Dkt. Mwinyi amesema nao watanufaika kwani wataweza kufungua
mashauri na kufuatilia uendeshaji wa mashauri yao wakiwa nyumbani, vijijini ama
ofisini na kwa njia hiyo wataweza kuutumia muda mwingi ambao hutumika kwenye
taasisi za sheria kuweza kufanya kazi zingine za kuinua vipato vyao.
“Kwa muhtasari, haki
mtandao ina mchango mkubwa wa kuimarisha uwazi, uwajibikaji, utawala bora,
ukusanyaji mzuri wa mapato na kuimarisha uchumi wa nchi. Aidha itasaidia kukuza
imani ya wananchi na wawekezaji wa nje na wale wa ndani kwa vyombo vya sheria,”
amesema.
Awali, akimkaribisha
Rais Mwinyi kuongea na wananchi, Jaji Mkuu wa Zanzibar alisema kuwa wamechagua
kauli mbiu hiyo kwa vile haki mtandao siyo suala linalohusu Mahakama pekee,
bali pia kila mdau anayejihusisha katika mnyororo wa utoaji haki nchini.
Amesema Mahakama
Zanzibar inatambua juhudi za Serikali za kuanzisha mifumo mbalimbali ambayo
imerahisisha utendaji wa kazi, hivyo wanaunga mkono juhudi hizo kwa kuanzisha mifumo
mbalimbali, ukiwemo ule wa kusajili Mawakili kwa njia ya mtandao na mfumo wa
kupandisha hukumu katika ZanzLii.
Jaji Mkuu amebainisha
kuwa matumizi ya TEHAMA yataondoa usumbufu wa wananchi wakati wa kutafuta haki
zao mahakamani, ikiwemo jinsi ya kufungua mashauri kwa njia ya mtandao na
kupata hukumu kwa wakati, kupunguza muda wa kushughulikia mashauri na kuongeza
uwazi, hivyo kuimarisha imani kwa Mahakama.
Maadhimisho hayo yalianza
majira ya saa 2.30 asubuhi kwa wageni waalikwa na wananchi kuwasili katika
viwanja vya Mahakama Kuu Tunguu.
Mhe. Prof. Juma
akiongozwa na mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Zanzibar, aliwasili katika viwanja
hivyo majira ya saa 3.15 asubuhi akiwa ameongozana na viongozi wengine wa
Mahakama ya Tanzania na wale kutoka Zanzibar.
Rais Mwinyi ambaye ndiye
aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo aliwasili katika viwanja hivyo
saa 3.40 na kwenda moja kwa moja kwenye jukwaa kuu na kukaribishwa na viongozi
mbalimbali wa Serikali na Mahakama.
Baadaye Nyimbo za Taifa,
Zanzibar na Jumuiya ya Afrika Mashariki zilipigwa kabla ya viongozi wa dini
kuiweka shughuli hiyo mikononi mwa Mola.
Baada ya utenzi maalumu
uliokuwa umeandaliwa kusherehesha maadhimisho hayo kuimbwa, viongozi mbalimbali
walipewa nafasi ya kuwasilisha salamu, wakiwemo Rais wa Chama cha Mawakili
Zanzibar, Mkurugenzi wa Mashtaka visiwani humo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
wa Zanzibar.
Viongozi wa Mahakama ya
Tanzania waliohudhuria maadhimisho hayo ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sylvester Kainda.
Majaji wa Mahakama Kuu Zanzibar wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akipandisha Bendera ya Mahakama Zanzibar baada ya kuizindua. Chini ni picha ya Nembo ya Mahakama ya Zanzibar aliyoizindua.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (kushoto) akimkabidhi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi zawadi maalumu iliyoandaliwa na Mahakama kwa ajili yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni