Na Faustine Kapama-Mahakama, Zanzibar
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 12 Februari, 2023 ameshiriki kikamilifu
kwenye mbio za kilometa 10 za Siku ya Sheria zilizoandaliwa na Mahakama Zanzibar
kwa lengo la kuchangia waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mbio hizo zilizoanzia katika
maeneo ya Ngome Kongwe au Forodhani na kumalizikia katika Viwanja vya Mapinduzi
Square mjini Unguja zimeongozwa na Mke wa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi na kuhudhuriwa na
viongozi wengine wa Mahakama na Serikali.
Miongoni mwa viongozi wa
Mahakama ya Tanzania walioshiriki mbio hizo ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe.
Barke Sehel, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani,
Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel na Msajili Mkuu wa
Mahakama, Mhe. Wilbert Chuma.
Kwa upande wa Mahakama Zanzibar
waliohudhuria mbio hizo ni Jaji Mkuu, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Majaji
kadhaa wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Bw. Kai Mbaruk na Mrajisi, Bi.
Valentina Katema.
Akitoa salamu baada ya
kumalizika kwa mbio hizo, Mhe. Prof. Juma aliwaambia washiriki waliofurika
katika Viwanja hivyo kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasikiliza wananchi katika masuala ya
udhalilishaji na ukatili wa kijinsia.
Kadhalika, Jaji Mkuu akawaeleza
kuwa Mama Mariam Mwinyi, ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha
Bora Foundation inayojishughulisha pia katika kupinga vitendo vya ukatili wa
kijinsia, ana masikio ya kusikia na anawasiliza wananchi katika maeneo hayo.
“Ninachoweza kusema
kinachobaki ni sisi wadau katika mnyororo wa utoaji haki kuhakikisha kwamba
tunapambana na hayo yote ambayo viongozi wetu wameyaona,” alisema.
Akimkaribisha Mama
Mwinyi kuongea na wananchi katika Viwanja hivyo, Jaji Mkuu wa Zanzibar
aliwapongeza viongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kushiriki kwenye mbio hizo.
Amesema kiasi cha fedha kitakachokusanywa watakipeleka Zanzibar Maisha Bora
Foundation kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Jaji Mkuu huyo
akabainisha pia kuwa wamengundua imekuwa vigumu kwa wahanga wa vitendo hivyo
kupata fidia baada ya wahusika kutiwa hatiani na kufungwa jela. “Mtu akifungwa
miaka 30 jela mara nyingi halipi ile fidia anayoamriwa kutoa kwa mwathirika baada
ya kutiwa hatiani. Ndiyo maana katika Siku ya Sheria tumekuja na kauli mbiu hii
ili kuwasaidia wahanga hawa,” alisema.
Ameiomba jamii kushiriki
kikamilifiu katika kupambana na vitendo hivyo kwa kufika mahakamani kutoa
ushahidi ili Mahakama iweze kufanya kazi yake vizuri. Mhe. Abdalla
amewakumbusha wananchi kuwa Mahakama inaweza kumtia mtu hatiani kwa makosa hayo
iwapo shitaka hilo litathibitishwa bila kuacha shaka yoyote.
Akizungumza na wananchi
kupitia hafla hiyo, Mama Mwinyi ameipongeza Mahakama ya Zanzibar kwa kuja na
wazo hilo la kuwashirikisha kwenye mbio za Siku ya Sheria kwa lengo la
kuwasaidia wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kama ilivyo taasisi yake
ya Zanzibar Maisha Bora Foundation.
Mama Mwinyi ameeleza kuwa wamedhamilia kuielimisha jamii ili kupambana na vitendo hivyo vibaya na kuhimiza wananchi kushiriki kikamilifu kuvitokomeza. Amesema kuwa Serikali imechukua hatua kadhaa kupambana na vitendo hivyo, ikiwemo kutunga sheria mbalimbali zinazotoa adhabu kali kwa wanaotiwa hatiani na kuzuia dhamana kwa baadhi ya makosa ya aina hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni