Na Faustine Kapama-Mahakama, Zanzibar
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 11 Februari, 2023 amemtembelea Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika
Ikulu ya Zanzibar na kuzungumza naye masuala mbalimbali, ikiwemo uboreshaji wa
huduma za utoaji haki unaoendelea kutekelezwa na Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Prof. Juma na
viongozi wengine walioambatana naye waliwasili katika Ikulu Zanzibar majira ya
saa 4.00 asubuhi na kupokelewa vizuri na mwenyeji wake. Baada ya utambulisho
uliofanywa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,
Jaji Mkuu aliwasilisha salamu kwa mwenyeji wake na kuainisha mambo manane yaliyokuwa
yanahitajika kutafutiwa ufumbuzi, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Tume ya
Jaji Mark Bomani mwaka 1993.
Aliyataja mambo hayo ambayo
yanayohusu ucheleweshaji wa utatuzi wa migogoro, wananchi kupata fursa ya
kupata haki, rushwa na maadili, uharaka wa kutoa uamuzi, imani ya wananchi kwa
vyombo vya utoaji haki, uwezo wa wanaopewa dhamana ya kuwa Majaji, Mahakimu, Mawakili
na wengine, uchache wa watoa huduma kwa kulinganisha na mahitaji yaliyopo na mazingira
au miundombinu ya kutendea kazi.
"Sisi Mahakama baada ya kuona matatizo ni
makubwa tukaona ni vema tubadilishe mwelekeo kwa kuanzisha maboresho ambayo
tunaendelea nayo sasa. Kabla ya kufanya hivyo tulifanya self-diagnosis ambapo Taasisi ya REPOA ilifanya tathimini na kwa
kupitia tathimini hiyo Mahakama iliandaa Mpango Mkakati wake wa awamu ya Kwanza,"
Jaji Mkuu alimweleza Rais Mwinyi.
Alibainisha kuwa Mahakama
imekuwa ikiboresha huduma zake tangu uhuru ili kutekeleza lengo lake kuu la kikatiba
katika kutenda haki, lakini changamoto kubwa wanayokutana nayo ni namna ya
kujipanga katika kutoa haki kwa wananchi.
Baada ya kuwasilisha
salamu hizo, Mtendaji Mkuu aliwakaribisha maafisa wengine wa Mahakama ya
Tanzania, akiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Mkuu
wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha na Kaimu
Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw. Allan Machela kuwasilisha namna Mahakama ilivyojipanga
kukabiliana na changamoto hiyo.
Rais Mwinyi alionyesha
kufurahishwa na jitihada zinazofanywa na kuhimiza Mahakama ya Zanzibar kutafuta
namna ya kufuata mfumo huo ambao Mahakama ya Tanzania imeshaanza nao ili na wao
waweze kupiga hatua kama wenzao waliyofikia.
Kabla ya kuhitimisha
mazungumzo hayo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania alisisitiza umuhimu wa
kuwekeza nguvu kubwa katika kuitangaza Mahakama kwani maboresho mengi na
makubwa yamefanyika katika Mhimili wa Mahakama lakini bado haijajajulikana kwa
wananchi.
Prof. Ole Gabriel
alibainisha pia kuwa kutoka na mabadiliko yanayoendelea duniani bila maboresho
na matumizi ya TEHAMA, Mahakama haiwezi kufanya chochote. Kadhalika, alimweleza
Rais Mwinyi kuwa mahusiano yaliyopo kati ya pande mbili za Mahakama ni mazuri,
akagusia ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Pemba ambacho kinatarajiwa kukamilika
ifikapo Juni 2024.
Akihitimisha mazungumzo
hayo, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis
Ramadhan Abdalla ameshukuru ushirikiano unaoendelea kushamiri wa Mahakama pande
zote mbili. Amesema suala la kusarifu mifumo ya TEHAMA iliyopo ya Mahakama ya
Tanzania litapewa kipaumbele ili kuhakikisha Mahakama ya Zanzibar inatumia
mifumo hiyo.
Jaji Mkuu huyo
alibainisha pia kuwa maboresho ya Mahakama ya Zanzibar yameanza na kwa sasa wanaandaa
Mpango Mkakati wa Mahakama ili kuhakikisha azma iliyopo inatekelezwa.
Katika ziara hiyo, Jaji
Mkuu wa Tanzania aliongoza na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustapher Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Dkt. Angelo Rumisha, Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw. Allan Machela na Afisa
kutoka Kitengo cha Maboresho Mhe. John Chacha.
Waliohudhuria hafla hiyo
kwa upande wa Zanzibar ni Jaji Mkuu, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji wa
Mahakama Kuu, Mhe. George Kazi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Bw. Kai Mbaruk na
Mrajisi, Bi. Valentine Katema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni