·Asema maboresho yaliyofanywa ni mapinduzi katika mfumo wa utoaji haki
Na Faustine Kapama-Mahakama, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa hatua iliyochukua na kufikia mafanikio makubwa katika kuboresha
huduma za utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Dkt. Mwinyi ametoa
pongezi hizo leo tarehe 11 Februari, 2023 katika Ikulu ya Zanzibar alipotembelewa
na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na viongozi
wengine waandamizi wa Mahakama ya Tanzania.
“Mna
kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa ambayo mmeyapata,” Rais Mwinyi
alisema na kumwelekeza Jaji Mkuu wa Zanzibar, “Kwa sehemu kubwa to adopt mfumo huu
ambao wenzetu wameshaanza nao ili na sisi tuweze kupiga hatua kama ambayo wao
wamefika.”
Rais wa Zanzibar
ameonyesha kuridhishwa na mifumo ya utoaji haki inayoendelea kutekelezwa na
Mahakama ya Tanzania, ikiwemo mfumo wa kusajili mashauri kwa njia ya mtandao,
kupandisha nakala za hukumu kwenye mfumo maalumu wa Tanzlii, kuanzisha Mahakama
inayotembea, ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati.
“Hii mifumo yote, kuanzia
huu wa TanzLii, e-ofice, mobile court na mingine mingi inaonekana ndiyo moja ya
sababu kubwa ya mafanikio haya, kwa hiyo lazima na sisi twende huko, (...) tuchukue
yote ambayo yamefanyika huko yakaonyesha mafanikio, (....) haya ni mapinduzi
makubwa katika mfumo mzima,” alisema.
Amebainisha kuwa alipoingia
madarakani alitambua kufanya maboresho kwenye Serikali pekee hakutasaidia,
hivyo aliwaita wenzake na kukaa na Jaji Mkuu na kuagiza uboreshaji kufanyika
ndani ya Mahakama, akiamini ndiyo njia pekee itakayoifanya nchi kusonga mbele
kimaendeleo.
Rais Mwinyi alielezea
furaha yake kwa Mahakama upande wa Zanzibar baada ya kulichukulia suala hilo kwa
uzito wake na wameanza kufanya maboresho makubwa. “Wananipa taarifa kwamba mnashirikiana
kwa karibu, niseme tu kwamba kama kuna sekta katika muungano wetu yenye
ushirikiano wa karibu ni Mahakama kuliko sekta zingine, bila shaka inatokana na
watendaji waliopo,” alisema.
Mhe. Dkt. Mwinyi
aliendelea kusema, “Sasa sina uhakika, au tuombe Mungu muendelee kuwepo, maana
wakati mwingine kama hakuna mfumo wa kufanya mtu anayeingia asiwe na hiari mara
nyingi mambo yanaweza kurudi nyuma kwa sababu tu kaja mtu mwingine, lakini tuombe
kwamba hii iliyoanza itengenezewe mfumo ili tusirudi nyuma.”
Ameahidi kuendelea
kuiwezesha Mahakama ya Zanzibar hasa kwenye maeneo ya kuimarisha miundombinu ya
majengo na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo amesema ni
muhimu katika kuboresha na kuharakisha huduma za utoaji haki kwa wananchi.
Amepongeza hatua
zilizochukuliwa na Mahakama ya Tanzania kujenga Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Pemba,
jambo ambalo litasaidia kupunguza gharama katika Serikali yake ya kujenga
miundombinu hiyo.
“Tunashukuru sana kwa
ushirikiano mkubwa mnaowapa wenzenu wa Zanzibar na sisi kama Serikali tunaahidi
kwa yale yote ambayo yanahitaji msukumo wa Serikali tutakuwa tayari kuyafanya,”
alimwambia Jaji Mkuu wa Tanzania pamoja na viongozi wengine wa Mahakama
alioambatana nao.
Viongozi wengine ambao
waliambatana na Mhe. Prof. Juma kumtembelea Rais Mwinyi ni Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Mhe. Wilbert Chuma, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Dkt. Angelo Rumisha, Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw. Allan Machela na Afisa
kutoka Kitengo cha Maboresho Mhe. John Chacha.
Waliohudhuria hafla hiyo
kwa upande wa Zanzibar ni Jaji Mkuu, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, Jaji wa
Mahakama Kuu, Mhe. George Kazi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Bw. Kai Mbaruk na
Mrajisi, Bi. Valentine Katema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni