Na Faustine Kapama-Mahakama
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 10 Februari,
2023 amewaapisha wajumbe wapya wa Tume ya Utumishi wa Mahakama walioteuliwa
hivi karibuni.
Hafla hiyo ya uapisho
imefanyika katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa Serikali, Bunge na Mahakama ya Tanzania, akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Wajumbe hao wapya
walioapishwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, ambaye anaendelea
na wadhifa huo na Mawakili wawili wa Kujitegemea, Msomi Tom Nyanduga na Msomi
Docas Mutabuzi.
Mawakili hao wawili
wanachukua nafasi ya Msomi Kalolo Bundala na Msomi Genoveva Kato ambao
wamemaliza muda wao wa kuitumikia Tume hiyo.
Tume ya Utumishi wa
Mahakama inaundwa na wajumbe ambao Jaji Mkuu wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wajumbe wawili wanaoteuliwa na Rais.
Majukumu ya Tume
yameelezwa kwenye Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya
mwaka 2011.
Imeundwa na Ibara ya 112
(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, Tume hii
ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama
ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni