Na Magreth Kinabo –Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 8 Februari, 2023 amekutana
na uongozi mpya wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na kuahidi
kuendeleza ushirikiano uliopo ili chama hicho kiweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Sehemu
ya uongozi huo chini ya Mwenyekiti wake, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani
ya Tanzania, Mhe. Barke Sehel, ulifika ofisini kwa Jaji Mkuu jijini Dar es Salaam
majira ya asubuhi, lengo kuu likiwa kujitambulisha na kupokea maelekezo mengine
katika kuendeleza chama hicho.
Akizungumza
na uongozi huo, Jaji Mkuu ameahidi kuendeleza ushirikiano na chama hicho kwa
kuzingatia umuhimu wake katika Mahakama ya Tanzania. Amekishauri chama hicho
kufanya utafiti kwenye masuala mbalimbali, ikiwemo usawa wa kijinsia.
“Niko tayari kuendelea kushirikiana nanyi,
mnafanya kazi nzuri kwa maendeleo ya Mahakama ya Tanzania. Nawashauri mfanye tafiti
katika hili eneo la usawa wa kijinsia na tupo tayari kuwasaidia,” alisema.
Amekihakikishia
Chama hicho kuwa kitaendelea kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa na mtu
yoyote. “Fanyeni kazi zenu kwa uhuru, hamtaingiliwa na mtu yoyote,” alisema.
Kadhalika,
Jaji Mkuu amekishauri Chama hicho kuangalia uwezekano wa kuijumuisha Zanzibar katika
uongozi kwa kuzingatia mfumo wa uchaguzi uliopo kwa sasa hautoi nafasi kubwa
kwa wajumbe kutoka visiwani kuchaguliwa.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa TAWJA alimshukuru Jaji Mkuu kwa ushirikiano
aliouonyesha. Ameahidi kuwa wapo tayari kufanya utafiti kama alivyoshauri kwa kuwa
nguvu kazi wanayo. Aidha, uongozi huo umeahidi kushughulikia suala la
uwakilishi wa uongozi kutoka Zanzibar.
Katika
utambulisho huo, Mhe. Sehel aliongozana na viongozi wengine, wakiwemo Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Dkt. Zainabu Mango, ambaye ni
Katibu, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia
Temeke, Mhe. Martha Mpaze, ambaye ni Katibu Mwenezi na Hakimu Mkazi Mkuu wa
Mahakama kutoka Kibaha, Mhe. Nabrike Mbaba, ambaye ni Mweka Hazina.
Hivi karibuni, TAWJA ilifanya uchaguzi wa viongozi katika ngazi ya taifa. Viongozi wengine waliochaguliwa katika chama hicho walikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Victoria Nongwa, ambaye ni Makamu Mwenyekiti, Mhe. Patricia Lusinda kama Katibu Msaidizi na Mhe. Pamela Meena ambaye ni Katibu Mwenezi Msaidizi. Viongozi hao watadumu katika nafasi hizo kwa kipindi cha miaka miwili.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa TAWJA waliofika ofisini kwake kujitambulisha. Kutoka kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Martha Mpaze (Katibu Mwenezi), Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel (Mwenyekiti), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zainab Mango (Katibu) na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama kutoka Kibaha, Mhe. Nabrike Mbaba (Mweka Hazina).
(Picha na Faustine Kapama-Mahakama)
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni