Jumatano, 8 Februari 2023

WAKILI MSOMI BENDERA ATOA UJUMBE MAHUSUSI KUPITIA UTENZI

Na Mwandishi wetu-Mahakama

Wakili wa Kujitegemea, Msomi Capt. Ibrahim Bendera amewaomba wananchi kutatua migogoro waliyonayo kwa njia ya usuluhishi kwani kukumbilia mahakamani kuna madhira mengi, ikiwemo kutumia muda mwingi na huanzisha vita baina ya wadaawa.

Katika utenzi wake ulioimbwa katika maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa Kanda ya Dar es Salaam hivi karibuni, Msomi Bendera amewaalika wananchi kukutana na kupatana, kufanya vinginevyo kunaweza kuendeleza mgogoro na chuki.

Sehemu ya Utenzi huo inasema, “Madhila mnayapata, Kwanza ni muda kupita, Pili kuanzisha vita, Kesi kuishindania. Nenda rudi isokwisha, Chuki nzito kupandisha, Yauongeza mshawasha, Kesi kuishindania. Uchumi utapwelea, Uendelevu kupotea, Na muda mtauchezea, Kesi kuishindania.”

Msomi Bendera anaendelea kueleza, “Njooni tuwapatanishe, Mje tuwashirikishe, Mje tuwaunganishe, Kesi kuishindania. Ni bora usuluhishi, Bila kuweka uzushi, Ni kwa amani mtaishi, Usuluhishi kutumia. Msipo usuluhisha, Mgogoro hautokwisha, Na chuki mtajivisha, Usuluhishi kutumia.”

Kwenye utenzi huo ulioimbwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Lioness Miburani kutoka Temeke, Wakili huyo amewasihi wananchi kuanza na usuluhishi kwanza pale wanaposhindana kwa vile taratibu zilizopo, zikiwemo za kimira zinahimiza kupatana na siyo kugombana.

Akawahimiza wanasheria wenzake, kama wadau muhimu, kuwa katika mstari wa mbele kutumia usuluhishi wakati wa kutatua migogoro. Katika kukazia msimamo huo, Msomi Bendera anasema, “Wadau wa Mahakama, Wapo na wamesimama, Twashirikiana mema, Ya haki kusimamia. Wadau ni kina nani? Mawakili namba wani, Na wale serikalini, Ya haki kusimamia.”

Watanzania hivi karibuni waliadhimisha Siku ya Sheria kote nchini kama ishara ya kuanza mwaka mpya wa shughuli za kimahakama, huku ujumbe mkuu ukiwahimiza wananchi kupeleka mahakamani migogoro ambayo imeshindikana kukatuliwa kwa njia ya usuluhishi.

Kiongozi wa Wanafunzi wa Shule ya Msingi Lioness Miburani akiwasilisha utenzi kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi baada ya kuimbwa. Wengine wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Isaya Arufani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makala, Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Dkt. Zainab Mango na Jaji wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Asina Omari. Picha chini wanafunzi kutoka shule hiyo wakijiandaa kuimba utenzi huo.

Wakili Msomi Capt. Ibrahim Bendera (juu na chini), mtunzi wa utenzi huo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni