Jumanne, 7 Februari 2023

UTENZI WA SIKU YA SHERIA, KANDA YA DAR ES SALAAM, 2023

Na Wakili wa Kujitegemea, Msomi Capt. Ibrahim Bendera

SEHEMU YA KWANZA: UKARIBISHO

1.        Kanda ya Dar es Salaamu,

Yawaalika kwa hamu,

Muito wa mashamshamu,

Kwenye Wiki ya Sheria.

2.        Ni Kanda ya Mahakama,

Twawapa zenu heshima,

Hapa tulipo simama,

Kwenye Wiki ya Sheria.

3.        Mahakama ya Tanzania,

Ni mfumo wa kutumia,

Haki ipate timia,

Kwenye Wiki ya Sheria.

4.        Pamoja nao wenzetu,

Wana wawakilisha watu,

Wamefika mbele yetu,

Kwenye Wiki ya Sheria.

5.        Kanda hii nawambia,

Sheria twazingatia,

Tangu ilipoanzia,

Kwenye Wiki ya Sheria.

6.        Majaji na Mahakimu,

Watumishi wote humu,

Tuna piga balagumu,

Kwenye Wiki ya Sheria.

7.        Majaji walo mahiri,

Weledi kwa tafakuri,

Hukumu za kufikiri,

Kwenye Wiki ya Sheria.

8.        Mahakama jumuishi,

Ipo ina watumishi,

Na haki ndiyo utashi,

Kwenye Wiki ya Sheria.


SEHEMU YA 2: KAULI MBIU

9.        Mbiu ni ile ya mgambo,

Ikilia ina jambo,

Msipigane vikumbo,

Usuluhishi kutumia.

10.    Kauli mbiu ya leo,

Kukuza maendeleo,

Sheria zetu koleo,

Usuluhishi kutumia.

11.    Mgogoro utokeapo,

Pale popote ulipo,

Usiruke kama Popo,

Usuluhishi kutumia.

12.    Anza na usuluhishi,

Tafuta wapatanishi,

Usifuate ubishi,

Usuluhishi kutumia.

13.    Mila yetu kupatana,

Popote mnaposhindana,

Msifuate kugombana,

Usuluhishi kutumia.

14.    Ni bora usuluhishi,

Bila kuweka uzushi,

Ni kwa amani mtaishi,

Usuluhishi kutumia.

15.   Msipo usuluhisha,

Mgogoro hautokwisha,

Na chuki mtajivisha,

Usuluhishi kutumia. 


SEHEMU YA TATU: WAJIBU WA MAHAKAMA NA WADAU

16.   Mahakama ni Mhimili,

Mmoja ulio kamili,

Ina uwezo stahili,

Ya haki kusimamia

17.      Bunge na Serikali,

Nayo pia mihimili,

Katiba ilivyo nakili,

Ya haki kusimamia.

18.   Wadau wa Mahakama,

Wapo na wamesimama,

Twashirikiana mema,

Ya haki kusimamia.

19.   Wadau ni kina nani?

Mawakili namba wani,

Na wale serekalini,

Ya haki kusimamia.

20.   Taasisi mbalimbali,

Za karibu na za mbali,

Zote zenye uhalali,

Ya haki kusimamia.

21.   Mahakama na wadau,

Pamoja bila dharau,

Twazitimiza nahau,

Ya haki kusimamia.

22.      Leo ni Wajibu wetu,

Kuwaelezea watu,

Waweze kuthubutu,

Ya haki kusimamia.

 

SEHEMU YA NNE: KUKIMBILIA MAHAKAMANI

23.    Kesi za mahakamani,

Ni ngumu siyo utani,

Na mwenzako hampatani,

Kesi kuishindania.

24.    Mikataba mloanzia,

Hata hukutarajia,

Tofauti kuingia,

Kesi kuishindania.

25.    Madhila mnayapata,

Kwanza ni muda kupita,

Pili kuanzisha vita,

Kesi kuishindania.

26.    Nenda rudi isokwisha,

Chuki nzito kupandisha,

Yauongeza mshawasha,

Kesi kuishindania.

27.    Uchumi utapwelea,

Uendelevu kupotea,

Na muda mtauchezea,

Kesi kuishindania.

28.    Njooni tuwapatanishe,

Mje tuwashirikishe,

Mje tuwaunganishe,

Kesi kuishindania.

29.    Hii ndiyo Kanda yetu,

Yawahudumia watu,

Mkosaji asithubutu,

Kesi kuishindania.

______________________o0o____________________

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni