Na. James Kapele – Mahakama, Katavi
Ikiwa zimepita siku tano toka
kilele cha Siku ya Sheria kuadhimishwa nchini, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Sumbawanga imeanza vikao maalumu vya kusikiliza mashauri (sessions) ambapo
imepanga kushughulikia mashauri ya mauaji 13 mkoani hapa kwa muda wa siku 31.
Vikao hivyo vinavyoongozwa
na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Sumbawanga, Mhe. Thadeo Mwenempazi vimeanza leo tarehe 6 Februari, 2023 na vinatarajiwa
kuhitimishwa tarehe 7 Machi, 2023. Kati ya mashauri hayo 13, nane yatasikilizwa
na kutolewa uamuzi na mengine matano yanawahusisha washitakiwa ambao watasomewa
mashitaka yao kwa mara ya kwanza.
Awali, Mhe. Mwenempazi alikagua
gwaride liloandaliwa na kikosi cha kutuliza ghasia cha Jeshi la Polisi mkoani
Katavi kuashiria kuanza kwa usikilizwaji wa mashauri hayo kwa mwaka 2023.
Akiongea na waandishi wa
Habari waliohudhuria uzinduzi wa Vikao hivyo katika Viwanja vya Mahakama, Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Maira Kasonde amesema kuwa mpango
huo wa kuanza kusikiliza mashauri hayo kwa haraka ni kuhakikisha msongamano wa
mahabusu unapungua hasa kwa watuhumiwa ambao tayari mashauri yao yameshafikia
kwenye hatua ya kusikilizwa.
Amesema jumla ya vikao vitatu vya kusikiliza
mashauri vipepangwa kwa mwaka huu kwa lengo mahususi hilo hilo la kupunguza
msongamano wa mahabusu gerezani pamoja na kutoa haki kwa wakati.
“Tumepanga jumla ya mashauri
nane ya mauaji ya kusikilizwa kuanzia leo tarehe 6 Februari, 2023 mpaka tarehe
7 mwezi ujao kwa lengo la kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani. Kwa mwaka
huu tumepanga jumla ya vikao vitatu ili utimiza adhima hiyo.” alisema Mhe. Kasonde.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Thadeo Mwenempazi akipokea salamu za ukaguzi wa gwaride kutoka kwa kiongozi wa kikosi hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni