· Majaji na Mahakimu 170 washiriki
Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Mohamed Siyani amefungua Kongamano la Kimataifa linalohusu masuala ya Haki Miliki, Alama za Biashara na Usuluhishi wa Migogoro ya Miliki Bunifu ‘Judicial Colloquim on Copyrights, Trademarks and Mediation of IP Disputes’ huku akiwasisitiza Washiriki wa Kongamano
hilo kuwa na usikivu makini ili kushughulikia vyema migogoro inayohusu masuala
ya Haki Miliki.
Akifungua Kongamano hilo leo tarehe 28 Februari, 2023 kwa
njia ya Mkutano Mtandao ‘Video Conference’ akiwa ofisini kwake Mahakama Kuu
jijini Dar es Salaam, Mhe. Siyani amelishukuru Shirika la Umoja wa
Mataifa linalosimamia masuala ya Miliki Bunifu Duniani (WIPO) kwa kushirikiana kwa karibu na Mahakama
ya Tanzania kuandaa
kongamano linaloitwa “Judicial Colloquium on Copyright, Trademarks and Mediation
of IP disputes for the Judiciary of the United Republic of Tanzania”.
“Tukio la leo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano
kati ya Mahakama ya Tanzania na WIPO kwa lengo la kuimarisha mifumo na huduma
za Mahakama katika ulinzi wa miliki bunifu,” amesema Mhe. Siyani.
Alisema kuwa Miliki Bunifu (Intellectual Property) ni
jambo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yoyote hususani katika kipindi hiki
cha kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia, hivyo amesisitiza kuwa, ni muhimu kwa
Maafisa wa Mahakama kuwa na maarifa na uelewa wa kina kuhusu suala hilo.
Aidha; Jaji Kiongozi amebainisha kwamba, kwenye nchi
nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, kuna uelewa mdogo miongoni mwa Maafisa
wa Mahakama kuhusu masuala ya Miliki Bunifu ‘IP’, hivyo ana imani kuwa, kupitia
Kongamano hilo, litakalowapa nafasi ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu litasaidia
kuongeza uelewa pamoja na kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama kuhusu eneo hilo
muhimu.
Jaji
Kiongozi ameongeza kwa kulishukuru Shirika hilo kwa kuendelea kuwajengea uwezo
Majaji na Mahakimu wa Mahakama nchini, kuchapisha
maamuzi yanayohusu miliki Bunifu yanayotolewa na Mahakama ya Tanzania
kwenye mtandao wa ‘WIPO Lex Judgment Database’, uandaaji wa makongamano na semina mbalimbali na
kadhalika.
Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano hilo kwa njia ya Mkutano Mtandao
‘Video Conference’, naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uongozi wa
Mahakama ya WIPO, Bi. Eun Joo Min amesema Shirika hilo linashiriki katika kusaidia nchi
mbalimbali duniani kuwezesha kutatua migogoro inayohusiana na masuala ya Haki
Miliki.
Kadhalika, Bi. Eun ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana
kwa karibu zaidi na Shirika hilo na kuahidi kuwa Mafunzo zaidi yataendelea
kutolewa kwa Maafisa wa Mahakama.
“Tangu tumeingia katika makubaliano ya ushirikiano, Tanzania ni moja
kati ya nchi inayofanya vizuri, kwa mwaka jana mwezi Februari tuliweza kutoa Mafunzo
kwa Majaji na Mahakimu 60,” ameeleza Mkurugenzi huyo.
Katika siku ya kwanza ya Kongamano hilo, jumla ya Washiriki 170 wakiwemo
Majaji wa Mahakama ya Rufani (T), Majaji wa Mahakama Kuu, Wasajili na Mahakimu wameweza
kushiriki.
Kongamano hilo la siku tatu (3) lenye lengo la kuwajengea
uwezo Majaji na Mahakimu katika kushughulikia mashauri yanayohusu miliki bunifu litakuwa na Wawezeshaji mbalimbali kutoka Marekani, Uswisi, Uingereza, Tanzania, Taasisi ya Uongozi wa Mahakama ya WIPO na kadhalika, na Mada kadhaa zitatolewa ambazo ni pamoja na; Majukumu
ya WIPO na Kazi zake kwa Mahakama, Mifumo ya Kisheria na Haki Miliki za
Kimataifa na Kikanda, Jukumu la Mahakama katika uvumbuzi na Haki Miliki,
Masuala ya alama za Biashara katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria
za Kitaifa.
Shirika la WIPO lilianza kushirikiana
kwa karibu na Mahakama ya Tanzania tangu mwaka 2018 ambapo hivi sasa
wanashirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo uandaaji wa
majumuisho ya sheria na maamuzi yanayohusu miliki bunifu,
uaandaji wa nyenzo za kufundishia (Training Materials) na Utatuzi wa
Migogoro kwa njia usuluhishi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni