Jumanne, 28 Februari 2023

MAHAKAMA KANDA YA KIGOMA YATOA MOTISHA KWA WATUMISHI WAPYA

Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma

Mahakama Kanda ya Kigoma itaendelea kutekeleza kwa vitendo mkakati wake wa kutoa motisha za aina mbalimbali kwa watumishi wake wapya ili wasitamani kuhama kutoka katika Kanda hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha aliyasema hayo katika hafla iliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Hoteli ya Lake Tanganyika mjini hapa.

“Kanda ya Kigoma ni mahali pa zuri sana kufanyia kazi. Nawasihi watumishi wote, hasa mliopata nafasi ya ajira mpya na kupangiwa vituo vya kazi katika Kanda hii na wengine mliohamia kutosikiliza maneno ya watu kuwa Kigoma sio pazuri,” alisema.

Jaji Mfawidhi huyo aliendelea kusema, “Msifikirie kuhama kwa kuwa mazingira ya kazi ni mazuri, usalama ni mzuri na sisi viongozi na watumishi wenzenu tunawapenda. Tunawategemea sana ili kuunganisha nguvu na jitihada kuwezesha haki inatolewa kwa wakati na haraka kwa wananchi wote wanaohitaji huduma hiyo.”

Katika hafla hiyo, Mhe. Mlacha alikabidhi zawadi mbalimbali, zikiwemo pesa tasilimu, vitambaa vya suti na vitege kwa watumishi 22 wa ajira mpya, watumishi wanne waliohamia, watumishi wanne walioteuliwa kuongoza Mahakama za Wilaya na wengine nane waliostaafu utumishi mwaka 2022.

Hafla hiyo pia ilitumika kama nafasi ya kumuaga rasmi Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Fredrick Manyanda aliyehamia Kanda ya Tanga na kumkaribisha Jaji mwingine wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Stephen Magoiga aliyehamia katika Kanda hiyo ya Kigoma kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara.

Aidha, watumishi nane waliostaafu utumishi mwaka 2022 waliagwa rasmi na pia watumishi wanne walioteuliwa katika nafasi za Hakimu Mkazi Mfawidhi katika Mahakama za Wilaya Kibondo, Uvinza, Buhigwe na Kakonko katika Kanda hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Magoiga aliomba utamaduni huo mzuri uendelee maana unaleta motisha na kuongeza morali ya kazi katika vituo vya kazi. Aliwataka watumishi kwenda kusimamia vigezo vya utendaji, hususani suala la kuimarisha maadili, kuchapa kazi na kuwahudumia wananchi kwa weledi mkubwa.

Wageni mbalimbali walihudhuria hafla hiyo, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Salum Kalli.Wengine ni viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama Wilaya na Mkoa,wakuu wa Taasisi za Serikali na binafsi ambao ni wadau wa haki jinai na madai, wafanyabiashara, Mahakimu, Mawakili, watumishi wa Serikali na wale wa Mahakama kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Kigoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akizungumza na watumishi na wageni waalikwa kwenye hafla ya kuwakabidhi zawadi watumishi wapya na wale waliostaafu utumishi kwenye Kanda hiyo iliyofanyika hivi karibuni mjini Kigoma. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe Stephen Magoiga  na kulia ni Mkuu wa Wilaya Kigoma, Mhe. Sallum Kalli.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe Stephen Magoiga akisisitiza jambo baada ya kupewa nafasi ya kuongea na hadhara hiyo. Kushoto kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha na Mkuu wa Wilaya Kigoma, Mhe. Sallum Kalli.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja. Kutoka kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Mrakimu Msaidizi wa Polisi Philimon Makungu, Mkuu wa Wilaya Kigoma, Mhe. Sallum Kalli, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe Stephen Magoiga.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akitoa zawadi kwa mmoja wa watumishi wapya, Bw. Japhet Katunzi, ambaye ni Msaidizi wa Kumbukumbu kutoka Mahakama ya Wilaya Kakonko.
Watumishi wapya walioajiriwa hivi karibuni katika Mahakama Kanda ya Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja katika hafla iliyofanyika hivi karibuni baada ya kupokea zawadi zao toka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (hayupo kwenye picha).

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni