Na. Lusako Mwang’onda- Mahakama Kuu Iringa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta amewaasa watumishi wa Mahakama Kuu kwenye Kanda hiyo
kuacha kufanya kazi kwa mazoea, bali watekeleze majukumu yao kwa weledi na
umakini wa hali ya juu.
Mhe. Mugeta alitoa wito huo hivi karibuni katika kikao
cha pamoja alichokifanya na watumishi hao. Aliwaeleza kuwa tegemeo la wana
Iringa na Watanzania kwa ujumla katika kuitafuta haki liko kwenye chombo cha Mahakama,
hivyo kila mtumishi ahakikishe anawajibika ipasavyo ili kutimiza matarajio ya
wananchi.
Ameonya kuwa hatamvumilia mtu yoyote mzembe
na mvivu kwenye kufanya kazi katika kipindi chake atakachohudumu katika Kanda
ya Iringa. Amesema ni wajibu wa kila mtumishi wa Mahakama kutekeleza kwa
umakini na waledi yale yote yampasayo kuyatekeleza kwa mujibu wa Kanuni za
Utumishi.
Jaji Mfawidhi huyo alisema Kanuni za Utumishi
zinamtaka kila mtumishi wa umma kuwa kazini asubuhi na mapema, yaani saa 1:30
na kutoka alasiri, yaani saa 9:30, hivyo hategemei kuona mtumishi yoyote
hazingatii muongozo huo.
Alitumia nafasi hiyo kujitambulisha kwao baada ya
kuhamishiwa katika Kanda ya Iringa akitokea katika Kituo Jumuishi cha Masuala
ya Familia Temeke mkoa wa Dar es Salaam.
Naye, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanazania katika Kanda
hiyo, Mhe. Angaza Mwipopo, akizungumza katika mkutano huo alisisitiza upendo
baina ya watumishi.
Alisema ni muhimu kwa watumishi kupendana wao kwa wao
na kuwapenda viongozi wao na viongozi nao kuwapenda wanaowaongoza. Jaji Mwipopo
alikazia kuwa sehemu yoyote yenye upendo na isiyo na mfarakano huwa na mafanikio
katika kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni