Na Magreth Kinabo
-Mahakama ya Tanzania
Mahakama ya Tanzania
imefanikiwa kupunguza Mlundikano wa mashauri kutoka asilimia 11 mwaka 2021 hadi
kufikia asilimia 6 Desemba mwaka 2022.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe
27 Februari, 2023 jijini Dodoma na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe.
Wilbert Chuma wakati akizungumza kwenye kikao cha mapitio ya bajeti ya nusu ya mwaka 2022/23 na uchambuzi wa bajeti ya
2023/24.Kikao hiki kitamalizika Ijumaa ya wiki hii.
Alisema mafanikio hayo ni
hatua kubwa ambayo Mahakama haijawahi kuyafikia na kuongeza kuwa yametokana usimamizi
wa vikao vya kusukuma mashauri na mikakati usikilizaji mashauri.
Mhe. Chuma aliwataka
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania kutoridhika na mafanikio waliyopata bali waangalie
jinsi watakavyoipeleka mbali zaidi Mahakama ya Tanzania kwa kuzuia kabisa mlundikano
wa mashauri.
Alisema wanapotekeleza
majukumu ya utoaji haki kwa wananchi wahakikishe wanaacha alama ambayo
watakumbukwa kwa utendaji kazi wao kwa vizazi vijavyo wakiwa mfano katika
Mhimili wa Mahakama.
Aidha Msajili Mkuu huyo
wa Mahakama alisema uimarishaji wa miundombinu ya majengo katika maeneo
mbalimbali hapa nchini ni vema ukachangia huduma bora kwa kwa wateja wa ndani na
nje.
Katika hatua nyingine
Mhe. Chuma alisema wakati wakiwa katika maandalizi ya bajeti mpya ni vema
wakapanga mgao wa fedha unaozingatia halisi ya takwimu ili kuwezesha malengo ya
utoaji haki kwa wananchi yasikwame.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka watumishi wote kuendeleza
ushirikiano ili kulinda mafanikio yaliyofikiwa.
Alisema ushirikiano miongoni
mwa Watumishi ambao ni Maafisa wa Mahakama na wasio Maafisa wa Mahakama
utawezesha kuongeza kasi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
‘‘Masuala ya bajeti ni
sehemu muhimu ya kupanga mipango. Mimi naamini mtatumia kikao hiki kupanga
mipango mizuri ili kufanikisha kazi hii kwa ufanisi, ambayo itasaidia kufikia
malengo ya taasisi tuliojikwekea,’’ alisema Prof. Ole Gabriel.
Mtendaji huyo aliongeza kwamba
mapitio hayo yawe chachu ya kuendelea kujifunza wapi makosa yametokea kwa lengo la kutafuta majibu sahihi ya
changamoto zinazojitokeza katika kufikia malengo.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akitoa maagizo leo tarehe 27 Februari 2023 kwa wajumbe kutoka mikoa na Kanda mbalimbali za Mahakama Kuu ya Tanzania wakati kikao cha mapitio ya bajeti ya nusu ya mwaka 2022/23 na uchambuzi wa bajeti ya 2023/24 kinachofanyika jijini Dodoma.Kikao hiki kitamalizika Ijumaa ya Wiki hii.
Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Ufuatiliaji Erasmus Uisso akitoa maeneo ya utangulizi leo kwa wajumbe kutoka mikoa na Kanda mbalimbali za Mahakama Kuu ya Tanzania wakati kikao cha mapitio ya bajeti ya nusu ya mwaka 2022/23 na uchambuzi wa bajeti ya 2023/24.
Baadhi ya wajumbe kutoka mikoa na Kanda mbalimbali za Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika kikao cha mapitio ya bajeti ya nusu ya mwaka 2022/23 na uchambuzi wa bajeti ya 2023/24 kinachofanyika jijini Dodoma kuanzia leo na kitamalizika Ijumaa ya wiki hii..
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akifungua kikao cha wajumbe kutoka mikoa na Kanda mbalimbali za Mahakama Kuu ya Tanzania leo wakati kikao cha mapitio ya bajeti ya nusu ya mwaka 2022/23 na uchambuzi wa bajeti ya 2023/24 kinachofanyika jijini Dodoma leo tarehe 27 Februari 2023 na kitamalizika Ijumaa ya wiki hii.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati mstari wa mbele) akiwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma (wa tatu kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania mara baada ya kufungua kikao cha mapitio ya bajeti ya nusu ya mwaka 2022/23 na uchambuzi wa bajeti ya 2023/24 leo jijini Dodoma.
(Picha
na Mahakama ya Tanzania)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni