·Awataka kuzingatia weledi usiotia shaka
·Asema Mahakama haiwezi kufanya maajabu kwa ushahidi dhaifu
Na Faustine Kapama –Mahakama,
Morogoro
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amewahimiza
waendesha mashitaka na wapelelezi kote nchini kutekeleza majukumu yao
kikamilifu kwa vile Mahakama haiwezi kufanya maajabu, ikiwemo kumtia hatiani
mhalifu kwa kuletewa shahidi dhaifu.
Mhe.
Ngwembe ametoa wito huo leo tarehe 27 Februari, 2023 alipokuwa
anafungua mafunzo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania, kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA),
kwa washiriki 250 ambao ni waendesha mashtaka na wapelelezi kutoka taasisi mbalimbali.
Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa maboresho awamu
ya pili.
Amesema
jamii huwa haiielewi Mahakama hata kidogo na tena hudhihakiwa pale ambapo jamii
inaamini mtu aliyeshitakiwa ni mhalifu na imeshuhudia akitenda uhalifu, lakini
anaachiwa. Amewaeleza washiriki hao wa mafunzo kuwa katika mazingira hayo, chombo
kinacholaumiwa ni Mahakama, jambo ambalo halipendezi hata kidogo mbele ya macho
ya jamii.
“Lakini
Mahakama ifanye nini kama hakuna ushahudi wa kuweza kumhusisha mtuhumiwa na
uhalifu anaotuhumiwa nao. Kama upande wa mashtaka umeshindwa kuleta mashahidi
wa msingi, Mahakama ifanye miujiza gani. Lakini pia, upande wa mashtaka
utaendesha vipi shauri kama upelelezi haukufanywa kama inavyotakiwa. Mwisho wa
yote, mchakato mzima wa haki jinai utakuwa kituko mbele ya jamii,” alionya.
Mhe.
Ngwembe ameeleza kuwa uwepo wa mafunzo
hayo ni majibu ya kilio cha Mahakama cha muda mrefu dhidi ya udhaifu wa
uendeshaji wa mashauri ya jinai unatokana na udhaifu wa upelelezi. Ametumia
nafasi hiyo kutoa shukrani
za pekee kwa Benki ya Dunia ambao chini ya mradi wa kuimarisha upatikanaji haki
unaomlenga mwananchi (Citizen Centric Project -CCP) umewezesha,
pamoja na mambo mengine, kufanyika kwa mafunzo hayo.
Jaji
Mfawidhi huyo ameeleza pia kuwa Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2025, pamoja na mambo mengine, inalenga kuwepo kwa
mazingira ya amani, usalama na umoja; utawala
bora na utawala wa sheria; uwepo
wa jamii iliyoelimika na inayojifunza na kujenga uchumi imara na
shindani.
Sambamba na hilo, amesema Mahakama imejiwekea dhima ya
kufanikisha umalizaji wa mashauri kikamilifu na kwa tija, hivyo upatikanaji
haki kwa wakati sio tu utaimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama, lakini pia vyombo
vya haki jinai na kuwepo kwa misingi bora ya amani na utulivu.
“Ni Imani yangu kwamba haki jinai haiwezi kupatikana
bila kuhakikisha tuna wapelelezi wenye ujuzi na weledi usio tia shaka na wako
tayari kutumia ujuzi huo kuhakikisha wale tu wanaotuhumiwa kufanya makosa
wanafikishwa mahakamani na haki yao wanaipata,” Mhe. Ngwembe alisema.
Amebainisha pia kuwa upelelezi na uendeshaji wa makosa
ya jinai ni wa kisayansi zaidi kuliko hisia na nadharia za kizamani na makosa
mengi yanathibitishwa kisayansi kwa kutumia ama DNA, vipimo vya kidaktari au
kwa kutumia wataalam wa utambuzi wa maandishi.
“Lazima nisema hapa kwamba siridhishwi na makosa mengi
yanayofikishwa mahakamani bila kuwa na upelelezi ulio kamilika, au kumkamata
mtuhumiwa na kumshikilia kwenye vituo vya polisi bila kuwepo kwa upelelezi wa dhati unao mhusisha mtuhumiwa,” Jaji Mfawidhi
huyo aliwaeleza washiriki hao wa mafunzo.
Amesema makosa yenye adhabu ya vifungo vya muda mrefu kama
ubakaji, ulawiti na mahusiano yaliyo haramishwa kwa sharia, yaani incest
by male, wakati mwingine yametumika kudhalilisha watu wasio na hatia,
hata ugomvi wa kifamilia hupelekea kuhusisha makosa ya namna hiyo.
“Pia tumeshuhudia matumizi mabaya ya vipimo vya
kitaalam kwa kuwatumia watu wasio na utaalam wa kutosha. Nashawishika kutoa ushauri kwa Serikali au
Bunge kutunga kanuni na vigezo vya wataalamu wanao weza kutoa ushauri wa kitaalamu
ambao utakubaliwa na Mahakama, kama walivyofanya India. Hivyo kuwepo kwa mafunzo kama haya ni
ukombozi katika tasnia ya haki jinai nchini,” alisema.
Mhe. Ngwembe alieleza pia
kuwa anatambua Kifungu cha 9 (1) (e) cha Sheria ya Mashtaka ya Taifa kinatoa
mamlaka kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kusimamia zoezi la upelelezi kwa
kuelekeza na kuongoza polisi na vyombo vingine vya upelelezi, pamoja na mambo
mengine, katika kupeleleza taarifa yoyote ihusuyo jinai na kutoa taarifa haraka
iwezekanavyo.
“Kwa uzoefu mashauri yanayochelewa
kwenye upelelezi ni pamoja na mashauri ya mauaji. Ipo mifano kwamba, ushahidi
uliopatikana wakati upelelezi wa makosa makubwa yakiwemo ya mauaji ulipatikana
ndani ya wastani wa siku 90, lakini zaidi ya siku 240 zilitumika kwenye
mawasiliano kati ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na vyombo vya uchunguzi kwenye
masuala mengine ambayo hayakugusa ushahidi. Ni vema kujifunza namna ya
kupunguza hali hiyo,” Jaji Mfawidhi huyo alishauri.
Awali akimkaribisha Jaji
Mfawidhi huyo kufungua mafunzo hayo, Naibu Msajili Mwandamizi, Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Arnold Kirekiano alizitaja taasisi zinazoshiriki mafunzo hayo ni Ofisi
ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa
za Kulevya, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori na Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu.
Alieleza kuwa washiriki
katika mafunzo hayo kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni 50, wapo 100 kuutoka
Jeshi la Polisi, 40 kutoka TAKUKURU, 35 kutoka TAWA, 16 kutoka Mamlaka ya
Kupambana na Dawa za kulevya, tisa kutoka kitngo cha kupambana na fedha haramu.
“Tunaamini kwamba kwa
ushirikiano wa wadau ambao Mahakama inashirikiana nao kupitia ofisi ya Msajili
wa Mahakama Kuu tutapata nafasi tena wakati mwingine ya kuangalia mafunzo siyo
tu kwa wadau wengine lakini pia hata katika maeneo ya kijiografia ambayo pengine
hayakuguswa katika mafunzo haya,” alisema.
Naye Mratibu wa Mafunzo
kutoka IJA, Mhe. Raymond Kaswaga ameeleza kuwa mafunzo hayo ya wiki nne yamewaleta
pamoja washiriki hao ili waweze kubadilishana uzoefu kuhusu utendaji kazi wao
wa kila siku, ikiwemo changamoto zinazotokana na kukua kwa teknoloji na
kubadilika kwa mbinu za uhalkifu na wahalifu.
Amesema kuandaliwa kwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maboresho ya Mahakama ambayo yanatekelezwa kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2021-203/2024) na ni utekelezaji pia wa Sera ya Mafunzo ya Taifa 2003 pamoja na Sera ya Mafunzo ya kimahakama 2019.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni