Jumamosi, 25 Februari 2023

JAJI MKUU AKUTANA NA VIONGOZI WA TAWJA KANDA YA ARUSHA

Na Faustine Kapama –Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 24 Februari, 2023 amekutana na viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu (TAWJA) waliopo katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Mhe. Prof. Juma alisema kuwa sura ya Mahakama ya Tanzania inaonekana kupitia kazi nzuri wanayofanya TAWJA.  Alisema anaelewa kuwa kazi nyingi wanazofanya ni za kujitolea, hivyo ameahidi Mahakama itaona namna ya kuongeza fungu kusaidia TAWJA. 

Jaji Mkuu aliwaeleza viongozi hao kuwa mwezi Octoba 2023 kutakuwa na Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini mwa Africa (SACJF) utakaofanyikia Arusha, hivyo waangalie ni namna gani wanaweza kushiriki kama wana TAWJA ili kutengeneza mtandao mpana hasa katika kupata ziara za kubadilisha na uzoefu (exchanging programme). Ameahidi kuwapa ushirikiano wa hali ya juu ili kuboresha taswira ya Mahakama.

Viongozi wa TAWJA waliopo Arusha, ambao ni wapya wa Kamati Kuu Taifa TAWJA ni Katibu Msaidizi, Mhe. Patricia Kisinda na Katibu Mwenezi Msaidizi, Mhe. Pamela Meena ambao katika hafla hiyo waliambatana na Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Butamo Philip, Mhe. Devotha Kamuzora na Mhe. Nyigulila Mwaseba pamoja na Naibu Msajili, Mhe. Judith Kamala na Mratibu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Maria Sambo. Lengo kuu la Viongozi hao kukutana na Jaji Mkuu lilikuwa ni kujitambulisha baada ya kuchaguliwa hivi karibuni kushika nafasi hizo.

Jaji Mkuu alikutana na uongozi mpya wa TAWJA wa Tanzania, chini ya Mwenyekiti wake, ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Barke Sehel tarehe 8 Februari, 2023 jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha. Katika hafla hiyo, baadhi ya viongozi wa TAWJA hawakuwepo na walikuwa na majukumu mengine ya kikazi, ikiwemo jijini Arusha.

Hivi karibuni, TAWJA ilifanya uchaguzi wa viongozi katika ngazi ya taifa. Viongozi wengine waliochaguliwa katika chama hicho walikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Victoria Nongwa, ambaye ni Makamu Mwenyekiti, Mhe. Patricia Lusinda kama Katibu Msaidizi na Mhe. Pamela Meena ambaye ni Katibu Mwenezi Msaidizi. Viongozi hao watadumu katika nafasi hizo kwa kipindi cha miaka miwili.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu (TAWJA) waliopo katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongea na viongozi hao.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimsikiliza  Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Mhe. Butamo Philip (wa kwanza kushoto).
 Viongozi wa TAWJA Arusha (juu na chini) wakiwa pamoja na Jaji Mkuu ofisini kwake.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni