Jumamosi, 25 Februari 2023

MAHAKAMA SPORTS MPIRA WA MIGUU DAR ES SALAAM YAUMANA NA TANROADS PWANI

Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha

Timu ya mpira wa miguu ya Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, leo tarehe 25 Februari, 2023 imekutana na timu ya TANROAD Pwani katika mechi ya kirafiki iliyofanyika  katika viwanja vya TAMCO  Kibaha Mkoa wa Pwani.

Akiongea wakati wa mechi hiyo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Taifa, Wilson Dede amesema mechi hiyo inalenga kujenga urafiki na taasisi mbalimbali na pia kutafuta timu itakayoshiriki katika mashindano ya Mei Mosi yatakayofanyika kuanzia terehe 16- 30 Aprili mkoani Morogoro.

Aidha Mwenyekiti huyo amesema mashindano ya Mei Mosi ni magumu zaidi ya yale ya SHIMIWI, hivyo amewaomba wachezaji kufanya mazoezi ili kuweza kufanya vizuri katika mashindano hayo. Aliongeza kuwa uongozi wa Mahakama Sports umeaanda bonanza ambalo litashirikisha timu kati ya sita mpaka nane.

Kwa upande wake, Mchezaji Charles Ndyetabula akiongea kwa niaba ya Meneja wa TANROAD Pwani, amesema sio mara ya kwanza kucheza na Mahakama, hivyo ushirikiano na urafiki wao udumu na mchezo wa haki (fair play) uendelee kwani mambo yanayotokea ndani ya uwanja sio ya kujali maana hakuna mchezo utakaochezwa bila kugusana.

Pamoja na timu ya Mahakama kufungwa goli 2-0, Kocha wa Timu ya Mahakama Spear Mbwembwe alisema mechi hiyo imekua nzuri tofauti na mechi iliyopita ambapo Mahakama washinda kwa magoli 4-2.

Baada ya mchezo huo kumalizika, watumishi wa Mahakama Pwani na watumishi wa TANROAD walijumuika pamoja kwa mazungumzo maeneo ya Katumba PUB kama sehemu ya kufahamiana zaidi.

Timu ya Mahakama ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi, kocha na baadhi ya watumishi.
Timu ya TANROAD pwani ikiwa katika picha ya pamoja.
Mwenyekiti wa Mahakama Sports Taifa Wilson Dede akifuatilia mchezo huo.
Kocha wa Timu ya Mahakama Sports Spear Mbwembwe akifuatilia Kambumbu hilo.

Wachezaji wa Mahakama, wachezaji wa TANROAD pamoja  watumishi wakiburuka pamoja maeneo ya Katumba Pub Kibaha.

 (Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni