Jumatano, 22 Februari 2023

JAJI MFAWIDHI BUKOBA AFANYA ZIARA KUKAGUA MAHAKAMA YA WILAYA KYERWA

Na. Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculate Banzi leo tarehe 21 Februari, 2023 amefanya ziara ya ukaguzi katika Mahakama ya Wilaya Kyerwa mkoani Kagera.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Banzi alisisitiza watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano na kuzingatia maadili na nidhamu ili kufanikisha malengo ya Kanda pamoja na kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi huyo amesisitiza kuwa ni muhimu kwa watumishi wa Mahakama hiyo kutoa huduma nzuri kwa wananchi na kulitunza jengo hilo.

Itakumbukwa jengo la Mahakama ya Wilaya Kyerwa ni mojawapo ya majengo mapya 18 yaliyozinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 25 Novemba, 2022. Uzinduzi wa majengo hayo ulifanyika katika Mahakama ya Wilaya Busenga mkoani Simiyu.

Viongozi wengine waliokuwapo katika ziara hiyo ya ukaguzi ni pamoja na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe Amworo Odira, Mtendaji wa Mahakama kutoka Kanda hiyo, Bw. Lothan Simkoko, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kyerwa, Mhe. Flavian Kubigwa pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo katika Wilaya ya Kyerwa na watumishi wengine.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculate Banzi akisalimiana na wafanyakazi wa Mahakama ya Wilaya Kyerwa mara baada ya kuwasili mahakamani hapo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kyerwa. Wengine walioketi kuanzia kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kyerwa, Mhe. Flavian Kubigwa, Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe. Oodira Amworo, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko na Afisa Tawala Mahakama ya Wilaya Kyerwa, Bw. Prudence Bitumbi.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni