Ijumaa, 3 Machi 2023

AWAMU YA KWANZA YA MAFUNZO HAKI JINAI YAHITIMISHWA

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Awamu ya kwanza ya mafunzo ambayo yemeandaliwa na Mahakama ya Tanzania na Chuo cha Uongozi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro, kuwaleta pamoja waendesha mashitaka na wapelelezi kote nchini ili kujadili mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya haki jinai, yamehitimishwa leo tarehe 3 Machi, 2023.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabliel Malata, kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Paul Ngwembe, amehitimisha mafunzo hayo kwa kuwapa vyeti washiriki 62 katika awamu hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Mhe. Malata alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha haki inatendeka na ili kulifanikisha hilo ni lazima kuwepo kwa ushirikiano mzuri baina ya wadau hao na Mahakama. “Sisi sote tunawajibika kumhudumia mwananchi, tumebeba haki za Watanzania, hivyo tusipowajibika kila mmoja katika nafasi yake ni sawa na kudhulumu haki za wananchi,” alieleza Mhe. Malata.

Akiguzia upande wa upelelezi, Jaji huyo alisema kuwa ni wakati wadau hao walioshiriki mafunzo hayo kuwa chachu ya mabadiliko na kuhakikisha upelelezi unakamilika kwa haraka, kwani kutokufanya hivyo ni chanzo cha zao la lawama kwa taasisi husika toka kwa Mhimili wa Mahakama. “Ni matumaini yangu kuwa elimu hii mtaitumia kutibu changamoto tulizokuwa tunazipata huku mahakamani,” alisisitiza.

Awali, wakati akimkaribisha Jaji huyo kufunga mafunzo hayo, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Arnold Kirekiano alieleza kuwa washiriki 62 wamepata mafunzo ya namna wadau wa haki jinai wanavyoweza kusaidia Mahakama kutimiza malengo yake ambapo miongoni mwa malengo hayo ni kutoa haki kwa wakati. Amesema Mahakama imejipanga kuwa ifikapo 2025 mashauri yatachukua siku 180 kwa Mahakama za Wilaya na siku 245 kwa Mahakama za Mkoa kumalizika.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Bw. Mbange Mgogo alitoa shukurani kwa waandaaji wa mafunzo hayo na kuahidi kuwa vyeti walivyotunukiwa watavithibitisha katika utendaji kazi na uwajibikaji. “Tumethaminiwa kupewa elimu hii ambayo imeleta mabadiliko upande wa fikra na utendaji kazi wetu, tunahaidi kuwa mabarozi huko tutakaporejea,” alisema.

Mafunzo hayo yalifunguliwa tarehe 27 Februari,2023 ambapo yanategemewa kutolewa kwa wadau 250 ambao watafika kwa awamu nne. Mafunzo hayo yatatolewa kwa wadau wa haki jinai kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori na Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe.  Gabriel Malata akizungumza na washiriki wa mafunzo ya haki jinai awamu ya kwanza (hawapo pichani) wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Meza kuu wakati wa kufunga mafunzo ya awamu ya kwanza ya haki jinai. Katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe.  Gabriel Malata. Kulia ni Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Arnold Kirekiano na kushoto ni Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Emmael Lukumai.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe.  Gabriel Malata akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo. 
Mmoja wa wahitimu hao akionyesha cheti chake baada ya kukabidhiwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe.  Gabriel Malata. 
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo awamu ya kwanza waliohitimu leo tarehe 3 Machi, 2023. 
 (Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam) 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni