·Awakumbusha
Makamishna wa Tume kubuni utaratibu wa kufuatilia utendaji kazi
Na Faustine
Kapama – Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama leo tarehe 4 Machi,
2023 amewaapisha Makamishna wapya wa Tume hiyo walioteuliwa hivi karibuni na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hafla hiyo ya uapisho imefanyika katika ofisi
ndogo za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizopo jijini Dar es
Salaam. Makamishna hao wapya ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe.
Dkt. Gerald Ndika, Wakili Msomi Tom Nyanduga na Wakili Msomi Docas
Mutabuzi.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye ni Kamishna wa Tume, Mhe.
Mustapher Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, ambaye ni Katibu wa Tume,
Prof. Elisante Ole Gabriel, Makatibu Wasaidizi wa Tume, Bi Enziel Mtei na Bi
Alisia Mbuya na watumishi wengine wa Tume hiyo.
Kulikuwepo pia na Makamishna wawili ambao
wamemaliza utumishi wao, Wakili Msomi Kalolo Bundala na Msomi Genoveva Kato. Kutoka
Mahakama ya Tanzania alikuwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma na Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji, Bw. Erasmus Uisso.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Prof.
Juma alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha
Tume ya Utumishi wa Mahakama.
“Baada ya kipindi cha miaka mitatu
kukamilika tulikuwa na hofu, pengine ingechukua muda mrefu kabla ya nafasi
kujazwa, lakini aliteua Makamishna watatu ambao wamewezesha mwendelezo wa
kufanya kazi za Tume bila kupumzika. Tunamshukuru sana kwa kutupa Makamishna wenye
historia (zilizotukuka),” alisema.
Aliwapongeza Makamishna hao wapya kwa kukubali
utezi huo kwa kuzingatia kazi wanayoenda kuifanya siyo nyepesi. Kadhalika aliwapongeza
Makamishna wanaomaliza muda wao wa kuhudumu katika Tume kwa kazi nzuri waliyofanya.
“Mnaweza kuona mchango wenu kwa kuangalia
yale mafanikio tuliyofanya, idadi ya Majaji tuliyopendekeza kwa Rais na idadi
ambayo ameikubali kuonyesha kwamba hatua za awali za mapendekezo zilifanyika
vizuri. Nakumbuka hata idadi ya Mahakimu katika kipindi chenu ilikuwa kubwa
sana. Kwa mwaka 2020/2021 tumeajiri takribani Mahakimu 200 au 300 na kuna
masuala ya maadili mengi ambayo mmeyashughulikia,” alisema.
Mwenyekiti wa Tume alitumia nafasi hiyo
kuwakumbusha Makamishna wapya kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi katika Tume,
hivyo hawatakuwa wanazungumzia maslahi yao binafsi wanapotekeleza majukumu
waliyopewa bali wazingatie maslahi ya wananchi kwa ujumla.
Amesema kuwa watumishi wa Mahakama ni
tofauti na wabunge au wanasiasa ambao kila baada ya miaka mitano hurudi kwa wananchi
kuomba ridhaa upya ya kuwatumikia.
“Sisi kama Mahakama Katiba inatulinda, hiyo
nafasi ya wananchi kuangalia utendaji kazi wetu hawana. Kazi yetu muhimu kama
Tume ni kuangalia utumishi na utoaji wa huduma unaotolewa na Majaji na Mahakimu
kwa niaba ya wananchi,” amesema.
Jaji Mkuu amesema kwa kuwa wananchi hawana
nafasi ya kuwaita watumishi wa Mahakama kama watakuwa wamekiuka masharti, Makamishna hao wapya wa Tume hawana budi kutumia hiyo nafasi vizuri katika kuibua maeneo
mengine ya kuboresha utumishi wa Mahakama.
Alieleza kuwa kila mwaka Tume huajiri
watumishi wapya na kupandisha vyeo, lakini haijapata nafasi ya kupata taarifa
za utendaji, ikiwemo kuchukua hatua kwa mtu aliyepewa ujaji, uhakimu, au usajili
anapokuwa ameshindwa au kiwango chake cha utendaji kimeshuka.
“Kwa sasa tumejikita zaidi kwenye utovu wa
maadili, lakini hatujaangalia kwenye utoaji wa huduma. Haya ni maeneo ambayo tunapaswa
kuanza kufikiria tuwe na utaratibu wa kuangalia utendaji wa mara kwa mara kwa kila
mmoja, siyo tu suala la mashauri, lakini pia mambo mengine yanayogusa haki kwa
ujumla,” alisema.
Kwa upande wao, Makamishna hao wapya kwa
nyakati tofauti tofauti walimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
uteuzi walioupata, hivyo wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viapo
vyao.
Nao, Makamishna waliomaliza muda wao wameshukuru
kwa kuaminiwa kuitumikia Tume hiyo. Kadhalika, wamewapongeza Makamishna wapya
na kuwahakikishia ushirikiano kutoka kwao ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Mmoja wa Makamishina hao alitumia nafasi hiyo kuiomba Tume kuangalia uwezekano
wa kutenga nafasi kadhaa za utumishi kwa ajili wa watu wenye mahitaji maalumu
kama sera ya Serikali inavyoeleza.
Tume ya Utumishi wa Mahakama inaundwa na
wajumbe ambao Jaji Mkuu wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji mmoja
wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzani na wajumbe wawili wanaoteuliwa na Rais. Mtendaji Mkuu wa Mahakama huingia kama Katibu wa Tume hiyo.
Majukumu ya Tume yameelezwa kwenye Ibara ya
113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikisomwa pamoja na
kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.
Imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, Tume hii ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni