Na Stephen Kapiga-Mahakama Mwanza
Kikundi cha wanawake
ambao ni watumishi wa Mahakama zilipo Mwanza mjini (Judicial Women Mwanza)
kuanzia Mahakama Kuu mpaka Mahakama za Mwanzo jana tarehe 3 Machi, 2023 kilitembelea
Kituo cha Kulelea Watoto waliotelekezwa cha Forever Angels na kutoa msaada wa
pesa na vifaa mbalimbali.
Watumishi hao ambao
waliambatana na Mlezi wao, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza,
Mhe. Monica Ndyekobora walifanya tendo hilo la huruma ikiwa ni siku chache
kuelekea Siku ya Wanawake inayosherekewa dunia kila siku ya tarehe 8 Machi.
Akiwakaribisha watumishi
hao katika Kituo hicho kilichopo maeneo ya Bwiru Wilaya ya Ilemela mkoani hapa,
Mkuregenzi Msaidizi wa Forever Angels, Bi. Leonola Sanga alisema kuwa Kituo
hicho tangu kilipoanzishwa mwaka 2006 mwezi Agosti kikiwa na mtoto mmoja
kimelea jumla ya watoto 420.
Amesema kwa sasa wapo
watoto 20 wanaolelewa. “Kituo hiki hasa kinashughulika na watoto kuanzia umri wa
mwaka 0 hadi miaka mitano na mara nyingi huwa tunapokea watoto waliotelekezwa
au kutupwa na wazazi wao,” alisema Bi. Sanga.
Alieleza kuwa katika
kushirikiana na idara ya ustawi wa jamii wamekuwa wakitoa taarifa ya kila mwezi
kuhusiana na maendeleo ya watoto wanaopokelewa katika Kituo hicho kuwezesha
idara hiyo kufanya uchunguzi kwa lengo la kuwatafuta wazazi au ndugu zao.
“Pindi wazazi au ndungu
wanapokosekana watoto hao huwa huru kuweza kufanyiwa utaratibu wa kuathiriwa
(adoption) kwa wale waliokidhi sifa za kisheria kuweza kufanya hivyo na mtoto
anapozidi miaka mitano huwa tunampeleka katika vituo vingine kwa ajili ya
kuendelea na masomo, kwani hapa tuna elimu ya awali tu,” Bi. Sanga alisema.
Kituo hicho kinaendeshwa
kwa kutegemea msaada wa kutoka kwa wafadhili nje ya Tanzania, hususani katika
nchi ya Uingereza, ambapo wafadhili hao hutoa gharama za kulipa mishahara ya
wafanyakazi na mahitaji mengine.
Akiutambulisha umoja huo
wa watumishi wa Mahakama, Mwenyekiti wa Kikundi cha Judicial Women Mwanza, Bi.
Irene Malamsha aliwapongeza wanachama wote kwa kujitolea sehemu ya kipato chao
na kuweza kurudisha kwa jamii kwa njia ya msaada katika Kituo hicho.
“Niwapongeze wote kwa
hiki ambacho tumefanikiwa kukusanya na kuleta kwa jamii na hasa hawa watoto
ambao wametelekezwa na wazazi wao, kwani si hawa watoto ndio waliopenda kuishi
katika vituo hivi. Ni jukumu letu kama mama kuweza kusaidia watoto kwa
kurudisha kiasi tupacho katika kipato chetu kwa njia hii,” alisema.
Kikundi hicho
kimefanikiwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali, ikiwemo sukari, mchele, mafuta
ya ngozi na mafuta ya kupika na vifaa vingine vyenye jumla ya kiasi cha
shillingi za Kitanzania 500,000/=.
(Habari
hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni