Na. Arapha Rusheke- Mahakama, Dodoma
Kamati ya Kanuni ya Jaji Mkuu wa
Tanzania hivi karibuni ilitembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma,
jengo la Makao Makuu ya Mahakama pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi
ya Majaji jijini hapa na kufurahishwa na miundombimu hiyo inayowekezwa na
Mahakama ya Tanzania.
Katika ziara hiyo, Kamati hiyo ilifurahishwa
pia na mabadiliko na maboresho yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania, hususani
eneo la miundombinu katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
katika utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji wa
Mahakama ya Rufani, Mhe. Rehema Mkuye alifurahi kujionea majengo hayo ya
kisasa, hususani jengo la Makao Makuu ya Mahakama ambalo tayari limeanza kutoa baadhi
ya huduma za kimahakama.
Wajumbe wa Kamati walioshiriki ziara
hiyo ni Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiwemo Mhe. Mkuye (Mwenyekiti), Mhe. Mwanaisha Kwariko (mjumbe),
Mhe. Lugano Mwandambo (mjumbe) na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt.
Juliana Masabo (mjumbe).
Wajumbe wengine waliokuwepo ni Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimaliwatu,
Bi. Agness Kavishe, ambaye ni mwakilishi. Aidha, ugeni
huo uliambatana na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Edward Rutakangwa, na
Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Bw. Yamiko Malekano.
Kamati hiyo iliambatana na wajumbe wa Sekretarieti akiwemo Mhe.
Kifungu Kariho (Katibu Mwenza), Mhe.
Hawa Mnguruta (Mjumbe) na Mhe. Daudi Kinywafu (Mjumbe). Wajumbe hao
walipokelewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe.
Gerson Mdemu pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni