·Anyoshea kidole gumba mfumo mpya wa kupokea maoni, malalamiko
Na
Faustine Kapama`– Mahakama, Morogoro
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amewahimiza watumishi
wote katika Kanda zote za Mahakama nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi na
uaminifu wa hali ya juu ili kuondoa viashilia vya rushwa na malalamiko ya
kiutendaji yanatotolewa na wananchi.
Mhe. Ngwembe ametoa wito huo
leo tarehe 6 Machi, 2023 alipokuwa anafungua mafunzo ya kushughulikia malalamiko kwa njia ya mfumo wa kielekroniki (e- complaint)
ambayo yamewaleta pamoja Naibu Wasajili na Watendaji kutoka Kanda zote za
Mahakama yanayofanyika katika Ukumbi wa Magadu mjini Morogoro.
Mafunzo hayo yanatolewa
baada ya Mahakama ya Tanzania kuanzisha mfumo mpya wa kisasa wa kielektroniki uitwao “Sema na Mahakama”
utakaotumika katika kutoa na kupokea maoni, maulizo na malalamiko (mrejesho) kutoka
kwa wananchi. Mfumo huu unatarajiwa
kurahisisha njia za uwasilishaji wa maoni kuongeza uwazi katika kushughulikia
maoni, malalamiko na kuweza kukusanya taarifa sahihi kutoka kwa wadau wa Mahakama,
wakiwemo wananchi.
“Mahakama kilikuwa ni
chombo cha kulalamikiwa kila mwaka. Sasa, kutokana na mapinduzi makubwa
yanayoendea kufanyika, tunataka Mahakama iwe chombo cha kupongezwa na siyo
kulalamikiwa na kusutwa. Nataka Kanda zote za Mahakama Tanzania tusisikie
lalamiko lolote la rushwa. Ili tuondokane na hili lazima tujikite pia kwenye
uelimishaji wa wananchi,” alisema.
Alitolea mfano wa Kanda
yake ya Mororogo ambapo baada ya kufanya utafiti wa kina hivi karibuni imebainika
malalamiko ya vitendo vya rushwa yanayopokelewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rusha (TAKUKURU) ni yale yanayohusu uelewa mdogo wa wananchi wa masuala ya
kisheria.
“Nilimwita Mkuu wa
TAKUKURU hapa Morogoro, nikakaa naye ofisini, nikamwambia aseme usafi wa Mahakama
katika Kanda nzima ya Morogoro ukoje. Nilimwambia aseme ukweli, asinifiche kitu
chochote. Aliniambia kwa sasa hajapokea lalamiko lolote za rushwa, isipokuwa
tuhuma ambazo zilichunguzwa na kubainika zinahusu uelewa mdogo kwenye masuala
ya kisheria,” alisema.
Mhe. Ngwembe alisema sasa
anauhakika Mahakama ya Tanzania
itafikia asilimia 80% au zaidi kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama ifikapo
mwishoni mwa mwaka 2025, kufuatia hatua mbalimbali zilizochukuliwa na
zinazoendelea kuchukuliwa katika kushughulikia changamoto zinazowakabili.
Ametaja hatua zilizokwisha chukuliwa na Mahakama ni pamoja
na kuanzisha mfumo huo maalumu wa kushughulikia maoni, maulizo na malalamiko
ya wananchi, hivyo malalamiko mengi waliyokuwa wanayasikia huko nyuma yatakuwa historia.
Jaji Mfawidhi huyo amebainisha pia kuwa sambamba na
kuwepo mfumo huo maalumu, watekelezaji muhimu wake ni hao Naibu Wasajili na
Watendaji ambao wamekusanyika kupata mafunzo hayo ili mfumo uliopo uweze
kutekelezwa ipasavyo katika Kanda zao.
“Ni imani yangu kuwa kupitia mafunzo haya mtapata ujuzi
wa usimamizi wa mfumo huu ili uwawezeshe kushughulikia maoni, maulizo na
malalamiko ya wananchi kielektroniki.
Tunatarajia kuwa baada ya
mafunzo haya mtakwenda kuwafundisha maafisa malalamiko walio katika Kanda zenu
na kwa ujuzi mtakaoupata, mtasimamia na kuhakikisha kuwa maoni, maulizo na
malalamiko yanawasilishwa na kushughulikiwa kwa wakati kupitia mfumo huu,”
alisema.
Mhe. Ngwembe alisisitiza kwamba lengo la kufikia asilimia
80% ya kuridhika kwa wananchi na huduma zinazozitolewa na Mahakama haliwezi
kufikiwa kwakuwa na mfumo mzuri wa kutoa na kupokea mrejesho pekee, bali kuwa
na maafisa wenye weledi na kujituma katika kutekeleza wajibu wao.
Hivyo anatarajia matumizi ya mfumo huo utamilikiwa na
kutumiwa ipasavyo na watendaji hao wenyewe na watawasimamia maafisa
malalamiko waliochini yao ili kuhakikisha wanaufahamu vyema na wanautumia
ipasavyo.
“Simamieni utekelezaji wake ili kuona kila maoni au
malalamiko yaliyowasilishwa yanashughulikiwa kwa wakati kwa mujibu wa Mkataba
wa Mteja ambao Mahakama tumejiwekea. Ninyi mkawe chachu ya kuutangaza mfumo huu
kwa umma na namna unavyofanya kazi ili waweze kuujua na kuutumia kikamilifu,”
alisema.
Akiwasilisha neno la shukrani
baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Naibu Msajili kutoka Idara ya Usimamizi na
Ukaguzi wa Shughuli za Kimahakama na Maadili, Mhe. Kinabo Minja alieleza kuwa
tafiti zilizofanyika mwaka 2015 zilionyesha kiwango cha wananchi kuridhika na
huduma zinazotolewa na Mahakama kilikuwa asilimia 61.
Alisema baada ya kuchambua
na kuingiza masuala mbalimbali yaliyoonekana kuwa na changamoto kwenya Mpango
Mkakati wa Mahakama na baadaye kufanyiwa kazi kikamilifu, kiwango cha wananchi
kuridhishwa na huduma za kimahakama kilipanda hadi asilimia 78 kwa mwaka 2019.
“Lengo kwa sasa ni
kuhakikisha tunaendelea kuboresha huduma zetu, tunawajibika kwa wananchi, ni
jukumu letu kuhakikisha wananchi wanaridhika na huduma tunazozitoa. Tumeshaangalia
yale waliyotulalamikia na yale ambayo tunahitaji kuyafanya. Sasa, utafiti
mwingine unafanyika, tunaamini kiwango kitaongezeaka na malengo yetu ni kufikia
asilimia 80,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni