Jumatatu, 6 Machi 2023

JAJI NGWEMBE AHIMIZA MATUMIZI YA SAYANSI KATIKA UPELELEZI

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe awasisitiza wadau wa Haki Jinai kuzingatia matumizi ya sayansi wakati wa upelelezi ili kuirahisishia Mahakama wakati wa kutafsiri sheria.

Mhe. Ngwembe ameyasema hayo leo tarehe 6, Machi 2023 wakati akifungua mafunzo ya kundi la pili la wadau wa Haki Jinai ambayo yanayofanyikia katika ukumbi uliopo ndani ya jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro. 

Mhe. Ngwembe alitolea mifano mbalimbali ya kesi ambazo ziliwahi kutolewa uamuzi mahakamani na namna ambavyo uchunguzi wa kisayansi ulivyotumika kuirahisishia Mahakama kutenda haki. 

“Sayansi inaweza kusaidia kuthibitisha kosa na nyie mkiitumia vyema ni rahisi kwetu Mahakama kutenda haki,” alisema Mhe. Ngwembe na kuongeza kuwa ni matumaini yake kupitia mifano aliyoitoa itakuwa chachu kwao katika kutenda haki ili wanaohusika kutenda kosa watiwe hatiani na wasiohusika waachiliwe na kuendelea na majukumu yao. 

Aidha, Mhe. Ngwembe aliwaasa kuutumia utaalamu huo watakaofundishwa ili kudhibiti uhalifu katika jamii na kumthibitisha mualifu wa kweli. “Nyinyi ni wadau muhimu mnaobeba dhima ya Haki Jinai, hakuna miujiza ambayo Mahakama inaweza kuifanya ikiwa upande wa upelelezi na mwendesha mashtaka hautotimiza majukumu yake ipasavyo,” alieleza Mhe. Ngwembe. 

Mafunzo haya ni mwendelezo wa yale yaliyofunguliwa tarehe 27 Februari, 2023, hii ikiwa ni kundi la pili ambapo yatawahusisha waendesha mashtaka na wapelelezi toka taasisi mbalimbali. 

Mafunzo hayo ambayo yamefadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa maboresho awamu ya pili yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), lengo ni kuwafikia washiriki 250. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo awamu ya pili ya wadau wa Haki Jinai.
Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Arnold Kirekiano akizungumza na washiri wa mafunzo  hawapo pichani).


Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (aliyekaa katikati), Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Arnold Kirekiano (kulia) na kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mmbando (kushoto) (juu na chini) ikiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.

Sehemu nyingine ya washiriki (juu na chini) ikiwa katika picha ya pamoja.

Sehemu nyingine ya  tatu ya washiriki (juu na chini) ikiwa katika picha ya pamoja.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni