Jumatatu, 6 Machi 2023

MAHAKAMA YA TANZANIA YAONYESHA DHAMIRA YA KWELI KUWAJALI WANANCHI

·Yaanzisha Sema na Mahakama mpya

·Ni mfumo wa kielekroniki wa kutoa, kupokea maoni, mrejesho

Na Faustine Kapama`– Mahakama, Morogoro

Mahakama ya Tanzania imeanzisha mfumo mpya wa kielekroniki (e-complaint) uitwao “Sema na Mahakama” utakaotumika katika kutoa na kupokea maoni, maulizo na malalamiko (mrejesho) kutoka kwa wananchi. 

Mfumo huu unatarajiwa kurahisisha njia za uwasilishaji wa maoni na kuongeza uwazi katika kushughulikia maoni, malalamiko na kuweza kukusanya taarifa sahihi kutoka kwa wananchi na wadau wa Mahakama kwa ujumla.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu pembeni mwa mafunzo yanayofanyika mjini Morogoro ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa Naibu Wasajili na Watendaji kutoka Kanda zote za Mahakama hapa nchini, Naibu Msajili kutoka Idara ya Usimamizi na Ukaguzi wa Shughuli za Kimahakama na Maadili, Mhe. Kinabo Minja amesema kuwa mfumo huo umeletwa ili kuimarisha mawasiliano kati ya Mahakama na mwananchi kuhusu huduma zinazotolewa katika mchakato mzima wa utoaji haki.

“Kwa kupitia mfumo huu, mwananchi anaweza kuwasilisha maoni, malalamiko au pongezi kwa Mahakama aidha kwa kutumia simu yake mwenyewe, kwa kuandika ujumbe mfupi au kwa kupiga. Lakini pia anaweza kwenda kwenye mfumo wenyewe kwa kupitia kompyuta yake au njia ya e-mail na kuliwasilisha,” alisema.

Amesema hapo awali hapakuwepo na mfumo wa kielektroniki uliokuwa unatumika kuwaunganisha wananchi na Mahakama katika kujua huduma zinazotolewa, hivyo ujio wake utaleta mapinduzi makubwa na kurahisisha mawasiliano ambayo yatawezesha kupatikana kwa taarifa sahihi na uwepo wa usimamizi mzuri wa kushughulikia malalamiko.

“Mfumo huu mpya wa Sema na Mahakama ni mpana zaidi, unajumuisha mrejesho unaopokelewa kupitia kituo  cha Huduma kwa Mteja na kupitia njia nyingine za uwasilishaji wa mrejesho wanazotumia wananchi, ikiwemo ujumbe mfupi wa maneno, email na nyingine,” Mhe. Minja alifafanua.

Alieleza kuwa ili kuboresha huduma na kupata taarifa nzuri na sahihi imewalazimu kuja na mfumo huo wa kielektroniki ambao pia utasaidia kuwa na usimamizi makini wa ushughulikiaji wa malalamiko.

Mhe. Minja alieleza kuwa ushughulikiaji wa malalamiko kwa njia ambazo siyo za kielektroniki wakati mwingine unachangamoto kwenye usimamizi. Amesema kuna Mahakama nyingi nchi nzima kuweza kufuatilia kila moja namna wanavyoshughulikia malalamiko na utoaji wa mrejesho kwa wananchi, hivyo itakuwa rahisi zaidi kama mfumo huo mpya utatumika.

“Mfumo wa kielekroniki unatusaidia mambo mengi, ikiwemo usimamizi mzuri na kurahisisha uwasilishaji wa malalamiko kuliko ile ya mwananchi kulazimika kuja mahakamani kwa ajili ya kuandikisha lalamiko lake. Mfumo huu pia unasadia katika kupata taarifa sahihi. Taarifa ikiwa katika hali ya kielekroniki haibadiliki badiliki. Pamoja na kurahisisha, mfumo huu vilevile unasaidia kuona kile kinachoendelea,” alisema.

Akifungua mafunzo kuhusu mfumo huo kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama yanayofanyika katika Ukumbi wa Magadu mjini hapa, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe alisema kuwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Mahakama katika kushughulikia changamoto mbalimbali zitaongeza kiwango cha imani ya wananchi kwa huduma zinazotolewa.

Amesema anaamini kupitia mafunzo hayo watapata ujuzi wa usimamizi wa mfumo huo ili uwawezeshe kushughulikia maoni, maulizo na malalamiko ya wananchi kielektroniki. “Tunatarajia kuwa baada ya mafunzo haya mtakwenda kuwafundisha maafisa malalamiko walio katika Kanda zenu na kwa ujuzi mtakaoupata, mtasimamia na kuhakikisha kuwa maoni, maulizo na malalamiko yanawasilishwa na kushughulikiwa kwa wakati kupitia mfumo huu,” alisema.

Mhe. Ngwembe alisisitiza kwamba lengo la kufikia asilimia 80% ya kuridhika kwa wananchi na huduma zinazozitolewa na Mahakama kwa mwaka 2025 haliwezi kufikiwa kwakuwa na mfumo mzuri wa kutoa na kupokea mrejesho pekee, bali kuwa na maafisa wenye weledi na kujituma katika kutekeleza wajibu wao.

Naibu Msajili kutoka Idara ya Usimamizi na Ukaguzi wa Shughuli za Kimahakama na Maadili, Mhe. Kinabo Minja akifafanua kuhusu mfumo mpya wa Sema na Mahakama katika mahojiano maalumu leo tarehe 6 Machi, 2023 mjini Morogoro.
Sehemu ya Naibu Wasajili na Watendaji (juu na chini) wanaopikwa na Mahakama kuhusu mfumo huo mpya. 

Sehemu nyingine ya Naibu Wasajili na Watendaji (juu na chini) wanaopikwa na Mahakama kuhusu mfumo huo mpya. 

Sehemu nyingine ya tatu ya Naibu Wasajili na Watendaji (juu na chini) wanashiriki mafunzo hayo. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni