Ijumaa, 31 Machi 2023

JAJI KIONGOZI AAGIZA MASHAURI YA MUDA MREFU YAPEWE KIMPAUMBELE

Na Tiganya Vincent-Mahakama, Dar es Salaam.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, amewaagiza Maafisa wa Mahakama hiyo wakiwemo Majaji, Naibu Wasajili na Mahakimu kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika kushughulikia mashauri ya muda mrefu.

Mhe. Siyani alisema hayo jana tarehe 30 Machi, 2023 alipofanya ziara ya kikazikatika Gereza la Mahabusu Segerea jijini Dar es Salaam ambapo pia alipata fursa ya kusikiliza kero za mahabusu hao.          

"Kesi iliyotangulia kuja iwe ya kwanza kupangiwa tarehe kwa ajili ya kusikilizwa na hata mashauri yaliyorudi kutoka Mahakama ya Rufani na kupata namba mpya nayo yapewe kipaumbele,” alisisitiza.

Aidha, kwa upande wa Mahakimu, Jaji Kiongozi aliwataka kuchapa kazi na kuhakikisha kuwa kila mmoja anamaliza kiwango cha mashauri aliyopangiwa kwa mwaka.

Aliwasisitiza Mahakimu hao kumaliza idadi ya mashauri waliyopangiwa kwa mwaka ambapo Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wanatakiwa kumaliza mashauri 260, wa Mahakama za Wilaya mashauri 250 na kwa upande wa Majaji wa Mahakama Kuu wanapaswa kumaliza mashauri 220.

Akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Gereza hilo, Jaji Kiongozi alipokea taarifa na baadae alikagua maeneo mbalimbali ya gereza, ikiwemo vyumba wanavyolala mahabusu na jikoni wanapoandaliwa chakula chao.

Aidha; katika taarifa zilitolewa na mahabusu wa kike na wa kiume wa gereza hilo, walimuomba Jaji Kiongozi kuwa, mashauri yaliyokaa muda mrefu mahakamani yapewe kipaumbele na upepelezi ukamilishwe kwa wakati.

Katika ziara hiyo Mhe. Siyani aliambatana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi na viongozi wa Mahakama ya Tanzania kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.

    Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (mwenye suti nyeusi kushoto) akisalimiana jana na Viongozi wa Gereza la Mahabusu Segerea jijini Dar es Salaam alipowasili katika eneo hilo jana tarehe 30 Machi, 2023 alipofanya ziara ya kuwatembelea Mahabusu. Nyuma yake ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi.

    Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (wa pili kushoto),  akibadilishana na Viongozi wa Gereza la Mahabusu  Segerea mara baada ya kumaliza ziara yake katika Gereza hilo jana.

    Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (mwenye tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Gereza la Mahabusu Segerea na Viongozi wa Mahakama alioambatana nao. Kulia kwa Jaji Kiongozi ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi.

(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni