Na Faustine Kapama, Mahakama-Bagamoyo
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 31
Machi, 2023 amefungua na kushiriki kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na
Mahakama ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi kuwajengea uwezo Majaji na Naibu
Wasajili katika mashauri ya usuluhishi.
Kikao kazi
hicho kilichofanyika mjini hapa kimehudhuriwa na Majaji kutoka Mahakama Kuu Divisheni ya Usuluhishi, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili na
Watendaji kutoka Mahakama hizo.
Akizungumza
wakati anafungua kikao kazi hicho, Mhe. Siyani aliwakumbusha viongozi hao kuwa Mahakama
ya Tanzania ndiyo chombo chenye wajibu kikatiba katika utoaji haki kwa wote na
kwa wakati.
Alisema lengo la nguzo ya pili ya Mpango
Mkakati wa Mahakama ni kuhakikisha kuwa mashauri mengi ya madai yanakwisha kwa
njia ya usuluhishi, hatua ambayo ni utekelezaji wa matakwa ya Katiba, Ibara ya
107A (2)(d), msisitizo ukiwa ni matumizi ya njia za usuluhishi katika kumaliza
migogoro baina ya pande mbili.
Jaji
Kiongozi alieleza kuwa, kwa kuzingatia wajibu huo na kwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na mlundikano wa mashauri mengi
ya madai, mwaka 2015 Mahakama ya Tanzania ilianzisha Kituo cha Usuluhishi kwa ajili
ya usuluhishi wa migogoro ya madai katika ngazi ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
salaam na Divisheni ya Ardhi.
“Kwa hiyo
uanzishwaji wa Kituo hiki ni njia mbadala ya kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani
ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika ngazi zote za Mahakama,” alisema Mhe.
Siyani.
Aliwakumbusha
ziara ya Jaji Mkuu wa Tanzania. Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma aliyoifanya Julai,
2022 katika Kituo cha Usuluhishi, kujionea shughuli zilizotekelezwa na kusisitiza suala la
usuluhishi kupewa nafasi kwa ngazi
zote za Mahakama kwa kuwa linaleta matokeo chanya baina ya pande zote mbili za
mgogoro.
“Jaji Mkuu
aliona kuwa Kituo cha Usuluhishi kinapaswa kufanya utafiti ili kubaini muda unaopotea
katika usuluhishi na kutoa mapendekezo ya kuboresha utaratibu huo. Sambamba na hilo,
alielekeza watumishi wa Kituo kupatiwa mafunzo ili waongeze uelewa zaidi kuhusu
masuala ya usuluhishi wa migogoro. Hivyo, leo ninayo furaha ninapoona tumekutana hapa
katika kikao kazi hiki kujengeana uwezo wa namna bora ya usuluhishi wa migogoro
baina wa wadaawa,” alisema.
Akimkaribisha
Jaji Kiongozi kufungua kikao kazi hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Divisheni ya Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma, alieleza kuwa hakuna
shaka Majaji na Naibu Wasajili kila mmoja wao ameshiriki katika usuluhishi na
baadhi yao wamekuwa wakifanya hivyo kwa muda mrefu wakiwa na au bila imani
chanya.
“Lakini, naamini
tunaweza kukubaliana sote kwamba tumekuwa na uzoefu mzuri pale wadaawa
wanaofika mbele yetu wanapofanikiwa kutatua migogoro yao kwa njia ya usuluhishi,”
alisema na kubainisha pia kuwa usuluhishi umekuwa njia maarufu zaidi ya
kusuluhisha migogoro kwa wakati, kwa gharama nafuu na kwa njia ya siri, kama
takwimu zinavyoonyesha.
Hata hivyo, Mhe.
Maruma alieleza kuwa katika mamlaka yetu, taarifa zilizopo hazishawishi kwani
kiwango cha mafanikio ya usuluhishi bado ni cha chini kwa asilimia 20% ikilinganishwa
na mamlaka zingine ambazo kiwango cha mafanikio ni zaidi ya asilimia 80% ya utatuzi
wa migogoro kupitia mchakato wa usuluhishi.
“Hii ni kutokana
na sababu za nje na ndani. Hata hivyo, kikao kazi hiki kitazingatia sababu za ndani
ili kuhakikisha kwamba mchakato wa usuluhishi unaendelea vizuri na kwa
mafanikio, hivyo ni muhimu kwa Majaji na Wapatanishi kufanya kazi pamoja kwa
ajili ya uboreshaji, kuna matumaini siku zijazo,” alisema.
Alisema kuwa uzoefu
wa miaka saba tangu Kituo cha Usuluhishi kianzishwe unatoa fursa ya kipekee kwao
kama Majaji na Naibu Wasajili kubadilishana uzoefu na maarifa, kujadili
changamoto wanazokabiliana nazo na kutambua maeneo ya kuboresha. Jaji Mfawidhi
huyo alieleza matumaini yake kuwa kwa kufanya hivyo, wanaweza kuweka mfumo bora
na imara zaidi wa usuluhishi.
Katika kikao kazi hicho, washiriki walijadili mada
mbalimbali, ikiwemo njia za usuluhishi kwa
mujibu wa sheria na mikakati ya
kiutendaji ya kukabiliana na changamoto za pamoja na kuhakikisha matokeo ya
mashauriano yaliyofikiwa yanafanyika ili kuboresha matumizi bora ya usuluhishi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni