Na. Mayanga Someke – Mahakama Kuu Sumbawanga
Kamati ya Ulinzi
na Usalama Mkoa wa Rukwa hivi karibuni ilifanya ziara katika Mahakama Kuu
Sumbawanga kujadili changamoto za ukatili wa kijinsia, hasa zile zinazowakumba watoto
katika Mkoa huo.
Katika ziara yake, Kamati hiyo ikiongozwa na Mkuu
wa Mkoa, Mhe. Queen Sendiga ilikutana na uongozi wa Mahakama chini ya Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amiri Mruma ambapo
mkutano kujadili changamoto hizo ulifanyika ofisini kwake.
“Mkoa wa Rukwa una changamoto za ukatili wa
kijinsia na watoto wa mitaani wamekuwa wengi, hii inachangiwa na kukosekana kwa
elimu kwa wananchi. Ukatili huu unawakumba sana watoto na wananchi hawataki
kupeleka masuala haya Polisi kuhofia urasimu,” alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Alibainisha
kuwa kama Mkoa lazima kuwe na mikakati ya kukomesha hali hiyo, ikiwemo ustawi
wa jamii kuandaa walimu rafiki kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi, kupata
askari wapelelezi watakaoshughulikia aina hiyo ya makosa, dhamana kutotolewa
kwa watuhumiwa wa makosa hayo na kuruhusu Waandishi wa Habari kutoa taarifa za
matokeo ya kesi hizo.
Akizungumza
katika kikao hicho, Jaji Mfawidhi alisema kuwa makosa hayo yanawagusa pia Mahakama
kama sehemu ya jamii na Mahakimu na Majaji wanaongozwa na sheria wanapaswa
kuzifuata kwa kutenda haki kwa wote.
“Kuna tatizo
pia katika upelelezi wa mashauri haya, wengi wao hawawezeshwi kifedha kufanya
upelelezi wa kina.Vipimo vya vina saba (DNA) havifanyiki ili kusaidia
kuthibitisha makosa haya. Sheria yetu ya Makosa ya Jinai inautaka upande wa
mashitaka kuthibitisha shitaka bila kuacha shaka yoyote, hivyo ni muhimu
Waendesha Mashtaka na Wapelelezi kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa. Madaktari
nao watekeleze majukumu yao kwa weledi wakati wanafanya uchunguzi wa makosa
haya,” alisema.
Hata hivyo,
Mhe. Mruma aliiambia Kamati hiyo kuwa dhamana ni haki ya kikatiba kwa
mshitakiwa kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya Katiba. Alisema suala la Waandishi wa
Habari kutoa taarifa za hukumu kwa umma halina tatizo na inaruhusiwa kisheria.
Jaji Mfawidhi
alizungumzia suala la utoaji elimu kwa umma kuhusu makosa ya ukatili wa
kijinsia na kwamba Mahakama ipo tayari kutoa maafisa wake ili kushiriki zoezi
hilo. Aliahidi kuwa Mahakama Kanda ya Sumbawanga ipo tayari kutoa ushirikiano
katika uendeshaji wa kesi za makosa ya ukatili wa kijinsia.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Amir Mruma akifafanua hoja zilizoibuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wakati wa kikao cha kujadili changamoto za ukatili wa kijinsia kwa watoto.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Bagamoyo)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni