Na Faustine Kapama, Mahakama-Bagamoyo
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, amewahimiza
Majaji, Mahakimu na wote wanaohusika katika kazi za usuluhishi na upatanishi
kuziba mianya yote inayosababisha ucheleweshaji wa utatuzi wa migogoro kwa njia
hizo ili kufikia mafanikio yanayotarajiwa.
Mhe.
Siyani ametoa wito huo leo tarehe 31 Machi, 2023 mjini hapa alipokuwa anafunga
kikao kazi cha siku moja kilichoandaliwa na Mahakama ya Tanzania, Kituo cha
Usuluhishi kuwajengea uwezo Majaji na Naibu Wasajili katika mashauri ya
usuluhishi.
“Mnalo
jukumu kama Majaji, Mahakimu na wote wanaoshiriki kwenye kazi hizi za usuluhishi
na upatanishi, mkiamua kwa dhati kuziba ile mianya midogo midogo mfanikio zaidi
yanaweza kufikiwa hata hapa kwetu (kama ilivyo katika nchi zingine duniani),”
alisema.
Kwa
mujibu wa Jaji Kiongozi, faida za upatanishi zinajulikana, hivyo ni wajibu wa
kila mmoja kuona umuhimu wa kufikia mafanikio yanayotarajiwa. Alisema upatanishi
umefanikiwa katika nchi nyingi, hivyo anaamini usuluhishi unaofanyika na
kufanikiwa uwe nje au ndani ya Mahakama una faida siyo tu kwa Mahakama bali pia
kwa wadaawa na nchi kwa ujumla.
Mhe.
Siyani amewaomba washiriki wa kikao kazi hicho kuzingatia yale yote
yaliyojadiliwa na kukubalika baada ya changamoto mbalimbali kubainishwa, maoni kadhaa
kutolewa na maazimio kufikiwa.
“Zipo
changamoto ambazo zinaweza kushughulikiwa mara moja na kila mmoja wetu. Ni matumaini
yangu kila mmoja atazifanyia kazi mara moja. Aidha, zipo changamoto ambazo
zinahitaji uongozi kuzifanyia kazi, ikiwemo zile za kisheria. Sekretarieti
ihakikishe inakamilisha kuweka vizuri maazimio na kuwasilisha kwenye uongozi
ili hatua zichukuliwe,” alisema.
Kadhalika,
Mhe. Siyani amewahimiza Majaji Wafawidhi na Naibu Wasajili kuimarisha usimamizi
kwenye Masjala zao baada ya kubaini mapungufu, ikiwemo majalada kuchukua siku
moja mpaka 10 kuwafikia. Anaamini hilo likifanyika kwa wasaidizi wa kumbukumu
na wale wanaohusika kuchukua majalada hayo kutoka masjala moja kwenda nyingine itasaidia
kutatua tatizo la ucheleweshaji.
“Binafsi naamini
yapo mengi yanaweza kufanyika ili kurahisisha na kujenga ufanisi katika
upatanishi. Tukiweza, kwa mfano, kuzuia mianya ya muda unaopotea kutoka jadala
linapoamriwa kwenda kwa Mpatanishi hadi kumfikia Mpatanishi mwenyewe na kuwaita
wadaawa kwa ajili ya upatanishi husika, tutakuwa tumepiga hatua katika mchakato
mzima.
Awali, akiwasilisha
mada katika kikao kazi hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Usuluhishi,
Mhe. Zahra Maruma alibainisha changamoto kadhaa wanazokumbana nazo wanapotekeleza
majukumu yao, ikiwemo uelewa wa pamoja wa
sheria na taratibu zake, kutokuwepo kwa miongozo na kanuni ya uendeshaji
wa hatua ya upatanishi, kukosekana kwa mfumo
mzuri wa mawasiliano kati ya Kituo na Masjala za Dar es Salaam na
Divisheni ya Aridhi na kutobadilika kwa mitazamo na utamaduni wa mazoea katika
utekelezaji wa hatua ya upatanishi.
Kufuatia hali hiyo, Mhe. Maluma amependekeza kuimarishwa kwa mifumo
ya mawasiliano inayosomana katika kushirikiana kupata taarifa na ufuatiliaji wa
hatua za upatanishi wakati wote ili kupima utekelezaji wake na kuharakisha
ukamilishaji wa mfumo utakaounganisha kituo na masjala zingine ili kurahisisha
upatikanaji wa taarifa, uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa
hatua hiyo.
Pia
ameshauri tahadhari za kuchukua mapema kabla ya kuanza matumizi ya Wapatanishi
wa kujitegemea ambapo menejimenti na uratibu wa mashauri yanayofikia hatua ya upatanishi
inaweza kuwa ngumu zaidi pale ambapo Mpatanishi na Jaji anayesikiliza shauri
watashindwa kuwa na uelewa wa pamoja na utekelezaji wa taratibu unaoeleweka.
Kikao kazi
hicho kimehudhuriwa na Majaji kutoka Mahakama Kuu Divisheni ya Usuluhishi,
Divisheni ya Ardhi na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili na
Watendaji kutoka Mahakama hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni